Sendeu akimkabidhi jezi Kavumbangu leo Jangwani |
Na Prince Akbar
MSHAMBULIAJI
wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu ametambulishwa rasmi leo
katika klabu yake ya Yanga, makao makuu ya klabu, makutano ya mitaa ya
Twiga na Jangwani, Dar es Salaam na kukabidhiwa jezi namba 21.
Akimtambulisha
mchezaji huyo, Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu alisema kwamba
mchezaji huyo kutoka Atletico Olympique ya Burundi, amesaini mkataba wa
miaka miwili.
Kavumbangu
amefanya mazoezi leo na wenzake Uwanja wa Loyola, Mabibo, Dar es Salaam
kujiandaa na Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Akizungumza
baada ya kutambulishwa kwenye mkutano huo, Didier alisema anashukuru
kutua Yanga, kwa sababu ni timu ambayo amekuwa akiisikia muda mrefu
tangu akiwa mdogo na atajitahidi kufanya vizuri, kuwafurahisha
mashabiki wa timu hiyo.
“Nimefurahi
kuja Yanga, nimefurahia mapokezi mazuri, na mimi naahidi nitafanya
vizuri kuwafurahisha mashabiki,”alisema Kavumbangu.
Katika
kikao hicho pia, mshambuliaji wa Yanga, Said Bahanuzi alikanusha uvumi
kwamba amesaini Simba. “Nina mkataba wa miaka miwili na Yanga, hizo
habari ni uzushi, mimi mchezaji wa Yanga,”alisema.
Yanga,
ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, walianza maandalizi yao
ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jana na Kocha Mkuu wa klabu hiyo,
Mbelgiji Tom Saintefiet aliwataja wachezaji ambao hawajaanza mazoezi ni
Hamisi Kiiza, ambaye ameitwa timu ya taifa ya Uganda, The Cranes,
Ibrahim Job na David Luhende ambao bado wapo kwao Mwanza, wakati Juma
Abdul bado ni majeruhi.
Tom
alisema wachezaji wengine waliokosekana mazoezini jana ni wale ambao
wapo timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro
Heroes, Frank Damayo, Omega Seme na Simon Msuva.
Yanga
ilitwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati, Jumamosi kwa kuifunga Azam
FC mabao 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wafungaji Hamisi Kiiza
‘Diego Milito’ na Said Bahanuzi ‘Spider Man’.
Hilo
lilikuwa taji la tano la michuano hiyo kwa Yanga kihistoria, baada ya
awali kutwaa mataji ya Kombe hilo katika miaka ya 1975 Zanzibar, 1993,
1999 Uganda na 2011 Dar es Salaam na mara zote hizo, ikiwa chini ya
makocha wa kigeni.
Mwaka
1975 Yanga ilibeba Kombe hilo, ikiwa chini ya kocha kutoka Jamhuri ya
Kodemokrasia ya Kongo (DRC), Tambwe Leya (sasa marehemu), 1993 chini ya
kocha kutoka Burundi, Nzoyisaba Tauzany pia marehemu, 1999 chini ya
Raoul Shungu kutoka DRC na mwaka jana chini ya Mganda Sam Timbe.
Wiki
hii ziliibuka habari kwamba, baada ya kuipa Yanga Kombe la Kagame,Tom
ameomba kazi ya kufundisha timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars,
lakini mwenyewe alisema baadaye akizungumza na BIN ZUBEIRY kwamba tangu amejiunga na klabu hiyo mwezi uliopita hajawahi kuomba kazi sehemu nyingine yoyote.
Mtakatifu
Tom alisema anashangazwa mno na habari hizo za kizushi, za kizandiki
zenye kulenga kumchonganisha yeye na mwajiri wake, Yanga SC.
“Nakumbuka
niliwahi kuomba kazi Chama cha Soka Kenya (KFF) kufundisha timu yao ya
taifa (Harambee Strars), lakini ilikuwa ni muda mrefu sana hata kabla
sijaomba kazi Yanga,”alisema.
Blog
moja iliyowahi kuandika Iddi Kipingu anagombea Uenyekiti Yanga, wiki
hii iliandika habari yenye kichwa kisemacho; “WIKI MOJA BAADA YA KUIPA
UBINGWA: KOCHA WA YANGA TOM SAINTFIET ATUMA MAOMBI YA KUIFUNDISHA
HARAMBEE STARS,”.
Akiizungumzia
habari hiyo, Mtakatifu alisema; “Ni uongo, tangu nimesaini mkataba na
Yanga, sijawahi kuomba kazi pengine popote,”alisema.
Sendeu katikati, kulia Kavumbagu kulia na Bahanuzi kushoto leo asubuhi . |
Didier Kavumbangu |
Comments