Na Salum Vuai, Maelezo
MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharibi,
amewataka wananchi wa Zanzibar kupuuza ushawishi wa baadhi ya watu na
vikundi, unaowataka wasikubali kuhesabiwa katika sensa ya watu na
makaazi inayotarajiwa kuanza Jumapili ijayo.
Akizungumza na waandishi wa
habari huko ofisini kwake Vuga, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, sababu za
kidini zinazotumiwa na vikundi na watu hao, hazina msingi kwani hakuna
dini inayokataza jamii au nchi kufanya hesabu ya watu wake.
Mwinyi ameeleza kuwa, zoezi la
sensa si kitu cha ajabu kwa Tanzania, kwani nchi zote duniani zinao
utaratibu huo unaofanywa kwa lengo la kufahamu takwimu za raia wao ili
kujua namna bora ya kujipangia mambo ya maendeleo na mahitaji ya msingi
yanayohitajika katika nchi hizo.
Aidha alisema, serikali zote
mbili za Tanzania na ile ya Zanzibar, hazijaona umuhimu wa kuweka
masuala ya kujua dini ya mtu kupitia zoezi hilo, kwani waumini wa dini
zote wana mahitaji na haki sawa za kuhudumiwa na serikali zao hizo.
Comments