Nimejitahidi
kutafakari ni kwa namna gani Katiba mpya itatuletea mabadiliko ya kweli
tunayoyataka, nimekosa majibu - na sidhani kama nitayapata.
Fikra
zangu zinanirejesha enzi za kudai Uhuru. Wapo walioamini kuwa kwa
kupata Uhuru, taifa letu lingepiga hatua kubwa kimaendeleo. Wapo
waliojiaminisha kuwa kwa kupata Uhuru, maana yake umasikini
ungetoweka.Wengine wakauona Uhuru kama mwanga wa kutufikisha kwenye
nchi ya kimaendeleo mithili ya Marekani na Ulaya. Bila shaka walikuwapo
walioamini kuwa kwa kupata Uhuru, basi kila kitu kinachomfaa binadamu
kingepatikana katika taifa letu.
Hizo
zilikuwa njozi. Miaka 50 baada ya Uhuru, tuna makabwela wengi
kupindukia. Idadi yao inaongezeka. Ile ahueni ya kuwapa Watanzania
elimu ya bure, maji bure, huduma za afya bure, imetoweka. Mambo
yanazidi kuwa magumu.
Ugumu
huu umewafanya wengi waamini kuwa kwa kupata Katiba mpya, basi kila
kitu kitakuwa kwenye mstari. Tunarejea tena kwenye njozi za Uhuru.
Wanaamini kwa kupata Katiba mpya, watapata milo mitatu kwa siku,
watasomesha watoto, watajenga nyumba, watanunua magari, watafanya kila
linalomfaa mwanadamu ili aweze kuishi kwa sifa zitakazomtofautisha na
wanyama wengine; na kwa kifupi ni kwamba Katiba mpya, mafisadi wote
watayeyuka kama theluji.
Kwa
nadharia hizi, naapa kwa dhati kabisa kwamba hata kama tutapata Katiba
mpya, itakuwa kazi bure. Wakati fulani aliyekuwa Rais wa Ghana, Jerry
Rawlings, alipata kuuliuzwa ni kwa namna gani ameweza kuifikisha nchi
yake kwenye maendeleo ya kupigiwa mfano.
Rais
Rawlings, akajibu kwa kujiamini kabisa kwamba ametumia sera za Tanzania
na maandiko ya aliyekuwa Rais wa Tanzania, Julius Nyerere, kuifikisha
Ghana hapo ilipofika. Akasifu maandiko na sera za Tanzania akisema
zilikuwa zimebeba mafunzo maridhawa kwa taifa lolote la Afrika kuweza
kuzitumia kwa mazingira yake na kujipatia maendeleo.
Huyo
alikuwa Rawlings. Yupo mwingine. Huyu ni Rais Paul Kagame wa Rwanda.
Kwa Kagame, Tanzania ni darasa tosha. Amekuwa muwazi kueleza mbinu
alizozitumia kuifikisha Rwanda hapo ilipo; nyingi akiwa amezinakili
kutoka kwetu. Nidhamu, utendaji kazi na kuyashusha maendeleo kwa
wananchi, ni mambo aliyoyazingatia. Haishangazi kuiona Rwanda ikiitumia
Oktoba 14 kama siku rasmi ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere.
Si
hao tu, bali yupo Rais Hugo Chavez wa Venezuela, ambaye kama ukiisema
vibaya Tanzania kwa sera zake, anaweza kukuadhibu! Nimepata kuhudhuria
Mkutano wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) katika jiji la
Havana, Cuba. Rais Chavez alitumia muda mrefu kumsifu Mwalimu Nyerere
na sera za Tanzania kwamba kama vikifuatwa, mataifa ya Kusini yatapiga
hatua kubwa kimaendeleo. Chavez ni mmoja wa wafuasi mahiri wa siasa ya
Ujamaa. Amehakikisha mali za umma zinabaki kuwa za umma. Zinawanufaisha
wananchi wote. Anatumia fedha za umma kusambaza huduma za kijamii kwa
wananchi wote bila ubaguzi. Ni mfuasi mkuu wa Mwalimu.
Waliofaidika
kwa sera za Tanzania ni wengi mno. Siwezi kuwataja wote. Ninachojaribu
kukisema hapa ni kwamba hata kabla ya Katiba mpya, Tanzania tumekuwa na
sheria na sera nzuri sana. Tumepata bahati ya kuwa na maandiko mazuri
na viongozi walioona mbali, lakini vyote tumevipuuza. Tumeviweka kando.
Sasa tunalilia Katiba mpya kana kwamba itakuja na kitu cha ajabu sana.
Kama
hatutabadilika na kuwa watu wa vitendo, hiyo Katiba mpya hata ikipambwa
kwa maandishi ya dhahabu na almasi, na ikafukizwa maradhi ya karafuu;
itakuwa kazi bure.
Katiba
ya sasa ukiisoma hutaona kama ina dosari nyingi za kuwafanya wengine
waisigine. Haina udhaifu huo. Katiba yetu imeeleza vema kabisa namna ya
kulinda rasilimali za nchi yetu. Imeeleza dhima ya kila Mtanzania
katika kulinda na kuhifadhi rasilimali asilia. Imeainisha haki ya kila
Mtanzania kutendewa haki mbele ya vyombo vya utoaji haki. Imesema
wananchi wote wako sawa mbele ya sheria.
Kutoka
na Katiba, tuna sheria nyingi. Tuna sheria hadi za kuzuia uvutaji
sigara katika hadhira-sheria ambayo haipo katika mataifa mengi duniani.
Tuna sheria za kulinda na kuhifadhi mazingira. Sheria hizo zikatungiwa
sheria ndogo ndogo zinazozuia kukata miti hovyo, kujisaidia maeneo
yasiyoruhusiwa, kutotupa taka ovyo, na kadhalika.
Pamoja
na utitiri wa sheria zote hizo, tujiulize, kitu gani kimetukwamisha
hata tusiweze kusitekeleza? Juzi, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) ametoa ripoti inayoonyesha namna Tanzania inavyotafunwa.
Sheria za kuwabana wezi zipo, tena zipo sheria kali kama ile ya Uhujumu
Uchumi. Kila mwaka CAG anatoa ripoti akiainisha majizi wanaolimaliza
taifa. Anafichua njama zinazofanywa na viongozi na wafanyabiashara
kuhakikisha Tanzania inasalia mifupa. Hakuna hatua zinazochukuliwa
dhidi ya wahusika. Hawachukuliwi hatua si kwa sababu Katiba ni mbaya,
au sheria hazipo, bali kwa sababu ya wanaopaswa kuifanya kazi hiyo kuwa
nao ni sehemu ya tatizo.
Ndiyo
maana najiuliza, hiyo Katiba mpya itakuja na upako gani utakaowafanya
Watanzania hawa hawa, wa tabia hizi hizi, na wa uporaji rasilimali huu
huu, wabadilike na kuwa watu tofauti? Silioni hilo.
Katiba
yetu hakuna mahali inasema wageni ndiyo wawe wa kwanza kufaidi
rasilimali za nchi. Haisemi wao ndiyo wafaidi samaki wetu maziwani na
baharini, lakini leo yote haya yanafanyika huku umasikini ukiongezeka
kwa wananchi. Kwenye sheria za nchi yetu ipo inayompa mamlaka rais
kuidhinisha mtu anyongwe. Hii ndiyo adhabu kali kabisa katika nchi
yetu. Wapo wanaoipiga vita kwa maelezo kwamba haisaidii kumaliza
matatizo. Wanasema inakinzana na haki ya msingi ya binadamu ya kuishi.
Sasa
kama hivyo ndivyo- kwamba sheria ya kuua ipo, lakini inatakiwa ifutwe-
sheria dhidi ya wahujumu uchumi ipo, sheria ya kufilisi mali za
mafisadi zipo, hiyo Katiba itakuja na jipya gani?
Ndiyo
maana nasema Katiba ya kweli ya Watanzania inapaswa kuandikwa katika
mioyo na utashi wao, na wala si ya kuandikwa kama hii tunayoililia sasa.
Tunapaswa
kubadilika kifikra. Tunapaswa kuwajibika-kila mmoja kwa nafasi
yake-tunapaswa kuwa watu wa vitendo zaidi badala ya blabla na porojo
zisizokoma, tunapaswa kusimamia sheria na kanuni tunazojiwekea.
Tunaweza kuwa na Katiba nzuri sana, lakini bila kuwa na wasimamizi wa kweli wa Katiba hiyo, tutabaki kuwa kichekesho.
Katiba
mpya na nzuri haitoshi kutufanya tushibe, haiwezi kuwasomesha bure
watoto wetu, haiwezi kupunguza ajali za barabarani kama madereva
wataendelea kubebwa, haiwezi kumaliza umasikini kama kila siku kazi
yetu ni kuamkia vilabuni na kushinda kwenye michezo ya “pool”. Katiba
mpya haiwezi kutufaa jambo kama wengi wetu tutakuwa tukisubiri kulishwa
chakula na mtu mmoja katika familia ya watu 15.
Wala
Katiba mpya haiwezi kutufaa lolote kama maono ya viongozi wetu ni
kuwahamasisha vijana kukopeshwa bodaboda badala ya kuwapa matrekta na
zana nyingine za kuwawezesha kuzalisha mali kwa njia za kisasa.
Katiba
mpya haiwezi kutufaa kitu kama tutaendelea kuabudu ushirikiana na
kuamini kuwa maendeleo ya mtu yanaletwa kwa imani za kijinga za kuwaua
ndugu zetu albino na kuchukua viungo vyao. Hatuwezi kubadilika
kimaendeleo kama tutabaki kuwa taifa la watu wanaoamini tunguli na
matangazo ya waganga matapeli eti wanaosafisha nyota na kutufanya
tupande vyeo kazini. Kama ingelikuwa kweli mtu akipata dawa hizo
anapanda cheo, basi kampuni ingekuwa na mawaziri 50 au 100 kwa wakati
mmoja!
Tuna
rasilimali ya mabonde, wanyamapori, madini, maziwa, bahari, mito, ardhi
isiyo na mfano; na ukwasi wa kila aina. Tunachohitaji si Katiba pekee,
bali viongozi makini wa kuwafanya wananchi wafaidike na ukwasi huu.
Kwangu mimi, suala la kuwabadili kwanza Watanzania kifikra ili waipende
nchi yao, wapende kuwajibika ndiyo yangekuwa mambo la maana zaidi
kwangu.
Tukiwa
na Katiba mpya, lakini tukawa na kiongozi anayemzuia Waziri kupanua
barabara eti kwa sababu kwa kufanya hivyo anawaudhi wapigakura, haki ya
Mungu tutaendelea kuonekana kama taifa ya washirikina tu.
Mwisho,
niseme kwamba Katiba “nzuri na tamu” haina maana kama uwajibikaji wa
viongozi wetu na wananchi vitakosekana. Je, uwajibikaji utaletwa na
maandiko tu; au kwa dhamira na utashi wa wenye nchi? Je, utaondoa
dhambi katika jamii kwa kujenga makanisa au misikiti mingi? Au
utapunguza dhambi kwa kuwabadili waumini kiroho? Unaweza kuwa na
makanisa na misikiti mizuri sana, lakini bila kuvitumia kwa maudhui
yake, itakuwa kazi bure. Yapo mataifa yasiyokuwa na Katiba
iliyoandikwa, lakini yapo mbele kimaendeleo. Nitakuwa wa mwisho kuamini
kuwa Katiba mpya ndiyo suluhu ya madhila yote yanayotufika sasa.
manyerere@hotmail.com
0759488 955
CHANZO: GAZETI LA JAMHURI
Comments