WAZIRI Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika, ameeleza kusikitishwa
na kauli za viongozi na watendaji wa Wizara ya Nishati na Madini na
Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kuhusu hali ya uzalishaji,
usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini sanjari na uboreshaji wa
utendaji TANESCO.
Amesema kauli hizo zinatoa matumaini potofu kwa wananchi na kuwasihi
kuzipokea kwa tahadhari kwa kuwa hazielezi ukweli kuhusu tatizo la umeme
nchini.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alitoa kauli hiyo jana katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari na kusema kulingana na nyaraka
alizonazo za ndani ya wizara hiyo na TANESCO kuanzia Septemba hadi
Oktoba mwaka huu, hali ya uzalishaji na usafirishaji na usambazaji wa
umeme imekuwa tete kwa sababu mbalimbali ikiwemo upungufu wa upatikanaji
wa mafuta na gesi asili kwa ajili ya uendeshaji wa mitambo ya kufua
umeme na kasi ndogo ya uwekezaji kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa kudumu.
Mnyika pia alisema amemwandikia barua Spika wa Bunge, Anne Makinda, ili
Wizara ya Nishati na Madini iwajibike kueleza hali halisi katika
mikutano ya kamati za Bunge inayoendelea.
“Katika barua hiyo nimependekeza pamoja na mambo mengine suala la
kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa mpango wa dharura wa umeme
na utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji wa TANESCO
lishughulikiwe na kamati nyingine kwa haraka kwa kuzingatia maelezo na
maelekezo ya Spika aliyoyatoa bungeni wakati wa kuahirisha mkutano wa
nane wa Bunge,” alisema.
Aidha alisema mapitio ya utekelezaji wa mpango wa uboreshaji wa utendaji
wa shirika hilo yahusishe kamati ya kudumu ya Bunge na itakayoeleza
hatua iliyofikiwa katika uchunguzi wa tuhuma za ufisadi kwa kuzingatia
kuwa siku 60 za uchunguzi zimepita.
Chanzo Tanzania Daima
Comments