Rwanda imechaguliwa kuwa kiti cha mwanachama wa muda wa Baraza la
Usalama la Umoja wa Mataifa, licha ya nchi hiyo kushutumiwa na jopo la
Umoja wa huo kuwaunga mkono waasi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Rwanda haikupingwa katika jitihada zake za kuwania kiti hicho kutoka
Afrika kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo Afrika Kusini
itamaliza muda wake mwezi Disemba mwaka huu, lakini bado ilikuwa
inahitaji idhini ya theluthi-mbili ya kura za wanachama wa Baraza Kuu la
Umoja wa Mataifa ili kupata kipindi cha muda wa miaka miwili. Rwanda
ilishinda baada ya kupata kura 148 kati ya 193.
Katika uchaguzi huo Argentina pia ilichaguliwa bila kupingwa baada ya
kupata kura 182, huku Australia ikishinda kwa kupata kura 140.
Luxembourg ilipata kura 131 na Korea Kusini kura 149.
Rwanda yazungumza baada ya kuchaguliwa
Baada ya kuchaguliwa katika chombo hicho cha Umoja wa Mataifa, Rwanda
imesema itafanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote wa baraza hilo
kuhakikisha inakuwa sikivu na kutafakari maoni na matarajio ya mataifa
yanayoendelea.
Kabla ya uchaguzi huo, ujumbe wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
uliliambia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuwa unapinga Rwanda kujiunga
na Baraza la Usalama la umoja huo, huku ikiituhumu nchi hiyo jirani kwa
kuwasaidia waasi wanaoendesha shughuli zao mashariki mwa Kongo.
Comments