Suzy Butondo, Shinyanga, MWANANCHI
RAIS Jakaya Kikwete amesema kuwa kuna wakati aliwahi kufikiria kuwanyonga watu waliokuwa wakikamatwa kwa kuhusika na mauaji ya albino yalipokuwa yamepamba moto kwa kuwa jambo hilo lilikuwa likimtia hasira.
Rais Kikwete alisema hayo jana katika kilele cha kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga. Rais alisema hayo alipokuwa akizungumzia tukio la uchomwaji wa moto makanisa lililotokea Mbagala, Dar es Salaam akieleza athari za mtu mwenye jazba kuchukua hatua. Juzi, Rais Kikwete alitembelea eneo la hilo la tukio na kushuhudia makanisa matatu yalivyoharibiwa pamoja na magari.
“Kwenye lile la maalbino nilishaandika kwenye hotuba yangu nitanyonga watu kwa kuwa nilikuwa nina hasira, lakini washauri wangu waliniambia hiyo itakuwa ni kinyume cha sheria kwa kuwa kuna watu walikuwa wamepelekwa mahakamani na hata uamuzi haujatolewa,” alisema Rais Kikwete na kuongeza: “Nilifuta baada ya kushauriwa, lakini hadi sasa nina hasira. Ninajitolea mfano wangu mwenyewe ili muone kwamba kujichukulia uamuzi kusivyokuwa vizuri wakati una hasira.”
Alirejea kauli yake kwamba kitendo cha mtoto kukojolea kitabu kitukufu cha Waislamu kilikuwa ni kosa kubwa na Waislamu walikuwa na haki ya kukasirika, lakini haikuwa sawa kwao kuvamia makanisa. Rais Kikwete alisema kitendo cha wao kuvamia makanisa na kuyachoma na kuvamia kituo cha polisi ni kinyume cha sheria za nchi.
“Mtoto mwenyewe kwanza hakutumwa na kanisa pia alikuwa mikononi mwa polisi. Sasa kitendo cha kwenda kituo cha polisi kutaka wapewe mhalifu wao ni kinyume cha sheria pia kuvamia makanisa ilikuwa si sawa.”
Akerwa na rushwa Katika hatua nyingine, Rais Kikwete amesema anakerwa na jinsi vitendo vya rushwa vinavyozidi kushamiri nchini na kutoa wito kwa Watanzania wote kushiriki kwa pamoja kuwafichua na kuwataja hadharani wale wote wanaojihusisha na tabia hiyo.
Alisema anachukizwa kuona vitendo vya rushwa vikizidi kushamiri, huku jamii ikikaa kimya bila kukemea kwa kuwafichua watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinachangia kwa kiasi kikubwa kuwanyima haki Watanzania walio wanyonge.
“Nawaombeni ndugu zangu tushirikiane kwa pamoja kupiga vita suala hili la rushwa, maana linaelekea kuota mizizi, ni wajibu wa kila mmoja wetu kujitoa muhanga kupiga vita ugonjwa huu wa rushwa.
Tuikemee sisi sote raia na wasio raia, watumishi wa umma na wasiokuwa watumishi wa umma, wafanyabiashara binafsi na wasiokuwa wafanyabiashara na kila mmoja awe ni balozi wa kupambana na vitendo vya rushwa.”
Mbio za Mwenge zilizinduliwa Mei 11, mwaka huu huko Mbeya na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda. Waumini wasali nje Siku tatu baada ya makanisa kuchomwa moto na kuharibiwa vibaya, baadhi ya waumini wamelazimika kusali wakiwa nje, huku viongozi wao wakiwataka kutolipiza kisasi kama mafundisho ya dini zao yanavyoelekeza.
Hata hivyo, viongozi hao wameitaka Serikali kutekeleza ahadi yake ya kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na uharibifu huo ili liwe fundisho kwa wengine. Juzi, Rais Kikwete alitembelea makanisa hayo na kuagiza polisi kuwasaka na kuwakamata wote waliohusika ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria. Jana, Mkuu wa Jimbo la Kusini la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Aman Lyimo alisema kwamba katika Usharika wa Mbagala, kamwe hawatalipiza kisasi dhidi ya waovu hao.
“Waliofanya kitendo hicho si Waislamu, bali ni wahuni wanaotumia dini kama kichaka cha kuficha uovu wao, tuliosomea dini mbalimbali tunafahamu kwamba hakuna dini yoyote inayoruhusu kufanya uovu kama huu uliofanywa katika makanisa.”
“Hatutawalaani wala kuwahukumu kwa sababu hawajui walitendalo, tutakachokifanya ni kuendelea kuwaelimisha bila kuchoka kwamba wanatakiwa kutubu kwa sababu wamemkosea Mungu.” Kiongozi wa Kanisa la Anglikana, Usharika wa Mbagala Kizuiani, Emmanuel Mng’ong’o alisema waumini wa kanisa hilo wamefanya ibada yao katika mazingira magumu baada ya vurugu hizo. Alisema madirisha 36 ya vioo vya kanisa hilo yalivunjwa, huku madhabahu ikiwa imeharibiwa...
“Tuna imani na ahadi ya Rais Jakaya Kikwete kwamba waliofanya uhalifu huo watachukuliwa hatua za kisheria.” Kamanda wa Mkoa wa Temeke, David Misime alisema jana kwamba hadi sasa jeshi hilo linawashikilia watu 122 kuhusiana na vurugu hizo.
CCM walaani Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimelaani kitendo cha kukojolea Kitabu cha Quran na uchomaji wa makanisa. Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema, “Vitendo hivi havifanani na utamaduni wetu Watanzania, wanaosifika kwa amani na utulivu.” Aliwataka wananchi kuwa na subira yanapojitokeza matukio kama hayo na kwamba vyombo vya dola vitachukua hatua stahiki kwa wote waliohusika.
Chanzo, MWANANCHI
Comments