ASHINDWA KUTETEA KITI MARA, AMPA ANGALIZO MSHINDI, TARIMBA ATAMBA DAR, WAMBURA ATUPWA
Waandishi Wetu
Makongoro Nyerere ameadhimisha vibaya kumbukumbu ya miaka 13 ya kifo cha
baba yake, Mwalimu Julius Nyerere baada ya kuangushwa kwenye uchaguzi
wa kuwania Uenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara uliofanyika juzi na kumalizika
usiku wa kuamkia jana.
Jana ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 13 tangu
kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere yaliyofanyika kwenye Uwanja
wa Kambarage, mjini Shinyanga yaliyokwenda sanjari na kuzimwa kwa Mwenge
wa Uhuru.
Katika uchaguzi huo wa Mkoa wa Mara, Makongoro aliyekuwa akitetea kiti
hicho, alipata kura 422 na kuzidiwa na mpinzani wake wa karibu,
Christopher Sanya aliyepata kura 481 huku tisa zikiharibika.
Uchaguzi huo ilibidi urudiwe kwa kuwashindanisha wagombea wawili, kwani
katika awamu ya kwanza wagombea wote hawakupata nusu ya kura kama kanuni
za chama hicho zinavyotamka.
Awali, katika nafasi hiyo wagombea walikuwa watatu. Katika awamu ya
kwanza, Sanya alipata kura 469, Makongoro (402) na mgombea mwingine,
Enock Chambiri aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoani Mara alipata kura
144. Baada ya matokeo hayo ya awali, Chambiri aliondoka ukumbini hapo.
Matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika katika Ukumbi wa CCM Mkoa,
yalitangazwa na Msimamizi Mkuu wa uchaguzi huo ambaye ni Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Nazir Karamagi.
Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Makongoro alisema kuwa anakubaliana
na matokeo hayo na kumuasa mshindi kufanya kazi kwa mujibu wa katiba.
Pia alimtaka mshindi huyo kuvunja makundi aliyosema yameshamiri ndani ya
chama hicho.
Comments