SIKU moja baada ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza (RPC),
Liberatus Barlow (52), kuuawa na kundi la watu wanaosadikiwa kuwa
majambazi, taarifa zinasema polisi wa kimataifa watashirikishwa kufanya
uchunguzi na kukamata wahusika wa tukio hilo.
Polisi mkoani Mwanza wameapa kupambana kuwasaka waliohusika katika tukio
hilo la kinyama, huku idadi ya watu waliokamatwa hadi kufikia Jumapili
jioni ikitajwa kufikia watu 15.
Kamanda Barlow enzi za uhai wake
Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zilizopatikana jijini Mwanza
zinaeleza kwamba, idadi hiyo ya watuhumiwa waliokamatwa huenda
ikaongezeka maradufu kuanzia kesho Jumatatu, baada ya marehemu Barlow
(pichani), kuagwa jijini hapa kesho kisha kusafirishwa hadi nyumbani
kwake Dar es Salaam, na baadaye Jumanne kusafirishwa nyumbani kwao
mkoani Kilimanjaro tayari kwa mazishi.
Kwa mujibu wa taarifa hizo ambazo baadaye Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani
Mwanza, Lily Matola pamoja na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai nchini
(DCI), Robert Manumba walikataa kutaja idadi halisi ya watuhumiwa
waliowakamata, zinadai kwamba upelelezi wa kina na wa hali ya juu
unafanyika kote nchini, ikiwa ni pamoja na maeneo ya mipakani ili
kuwanasa watuhumiwa wa mauaji hayo.
“Kazi ya kukamata watu wanaoshukiwa inaendelea. Na hadi leo Jumapili
zaidi ya watu 15 wameshakamatwa… na upelelezi wa kina unafanyika kila
kona ya nchi hii na hadi maeneo ya mipakani.
“Kuuawa kwa Kamanda Barlow si tukio dogo. Inahitajika nguvu ya ziada
kuwanasa watuhumiwa, ndiyo maana IGP Said Mwema amemtuma haraka sana
kuja Mwanza DCI Manumba. Ninyi subilieni tu mtasikia…wote waliohusika
tutawakamata tu”, kilisema chanzo cha habari kutoka ndani ya jeshi la
polisi mkoani Mwanza (jina tunalihifadhi).
Comments