Kwa
mara nyengine tena Rais Barack Obama ametajwa kumbwaga Mitt Romney
katika mdahalo wa televisheni, ambao licha ya mada yake kuu kuwa siasa,
masuala muhimu kwa wapiga kura, yaani uchumi na ajira, yalitawala
mjadala.
Safari hii, wachambuzi wanasema kwamba mpira ulikuwa unachezwa uwanjani
kwa Rais Obama - siasa za kimataifa - na hivyo alitumia vizuri ujuzi
wake kwenye eneo hilo kuponda kile kinachoonekana kama uelewa mdogo wa
Romney linapohusika suala la siasa za nje.
"Gavana Romney, nimefurahi kwamba unatambua kwamba al-Qaida ni tishio
kwa sababu miezi michache iliyopita ulipoulizwa ni kipi kitisho kikubwa
duniani kwa Marekani, ulisema Urusi, ilhali Vita Baridi vilimalizika
tangu miaka 20 iliyopita.
Linapokuja suala la sera za nje, unaonekana kurudisha siasa za miaka ya
1980, kama vile ambavyo una sera za kijamii za mwaka 1950 na za kiuchumi
za mwaka 1920. Unasema hupendelei kuigiza kilichotokea Iraq, lakini
wiki chache zilizopita ulisema unafikiria tuongeze wanajeshi zaidi
nchini Iraq." Obama alimdhihaki Romney.
Pakiwa pamebakia wiki mbili tu kabla ya Siku ya Uchaguzi, Romney
aliutumia mdahalo wa jana kushadidia hoja yake kwamba Obama ameufuja
uchumi wa Marekani
"Ili tuweze kuendeleza misingi hiyo ya amani, tunahitajika kuwa na nguvu, na hilo linaanza na uchumi imara hapa kwetu, na bahati mbaya uchumi si imara kiasi hicho.
Pale rais wa Iraq- samahani- rais wa Iran, Ahmedinejad, anaposema kwamba
deni letu linatufanya tusiwe tena taifa kubwa, hilo ni jambo la
kutisha. Mkuu wa zamani wa jeshi, Admirali Mullen, alisema kwamba deni
letu ndicho kitisho kikubwa cha usalama wa taifa. Tumeudhoofisha uchumi
wetu." Alisema Romney.
Comments