ACCRA, Ghana
MCHEZA filamu Juliet Ibrahim wa Ghana amesema majambazi
yaliyompora vitu vyenye thamani mbali mbali nyumbani kwake, ni
mashabiki wake wakubwa.
Juliet amewaelezea majambazi hao kuwa ni mashabiki wake
kutokana na kutomdhuru yeye na familia yake.
Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti hivi karibuni kuwa, Juliet
alikutwa na mkasa huo kwenye uwanja wa ndege wa Accra wakati
alipokuwa akirejea kutoka safarini Marekani.
Hata hivyo, Juliet alisema si kweli kwamba tukio hilo lilitokea
uwanja wa ndege. Alisema majambazi hao walimpora baada ya
kufika nyumbani kwake.
Alisema katika tukio hilo, majambazi hao walipora simu zao za
mkononi na pesa taslim, lakini hakuwa tayari kutaja thamani yake.
"Napenda kila mmoja afahamu kwamba, nipo katika hali nzuri mimi
na familia yangu na tukio la kuporwa lilitokea nyumbani, si uwanja
wa ndege,"alisema.
Kwa mujibu wa Juliet, tukio hilo lilitokea saa tatu usiku wakati
umeme ulipokuwa umekatika katika maeneo mengi ya Jiji la Accra.
"Kama kungekuwa na mwangaza, tungeweza kuwaona majambazi
hao walipoegesha gari lao jeusi. Nadhani katika kipindi hiki, kuna
matukio mengi yatakayotokea kwa sababu ya tatizo la kukatika kwa
umeme nchi nzima,"aliongeza.
Aliongeza kuwa, anachoshukuru ni kwamba yeye na familia yake
hawakupata madhara yoyote wakati wa tukio hilo.
"Natumaini majambazi hawa watakuwa wakisoma ujumbe huu.
Napenda kusema asante kwao kwa kutimiza maneno yao ya
kutoidhuru familia yangu. Ni mashabiki wazuri kwangu,"alisema
Juliet.
Comments