Na James Magai
Aliyekuwa Mbunge wa Sumbawanga Mjini
Aeshi Hilaly |
CHAMA Cha Mapinduzi(CCM), kimepata pigo jingine kisiasa baada ya
Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa ya aliyekuwa Mbunge wa
Sumbawanga Mjini, Aeshi Hilaly ambaye alivuliwa wadhifa huo na Mahakama
Kuu Kanda ya Sumbawanga.
Pigo hilo limekuja miezi miwili baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Tabora,
kutengua matokeo ya ubunge Jimbo la Igunga yaliyompa ushindi mgombea
wake, Dk Dalaly Peter Kafumu, Agosti 21, mwaka huu.
Rufaa ya Hilaly ilitupiliwa mbali katika uamuzi uliotolewa na jopo la
majaji watatu, Januari Msoffe, Edward Rutakangwa na Engela Kileo, baada
ya kubaini kasoro za kisheria.
Dosari hiyo ni kutokuwapo kwa mwenendo wa maombi ya mlalamikaji katika
kesi ya msingi ya kuomba Mahakama impangie kiwango cha fedha ambacho
alipaswa kulipa ikiwa ni amana ya kufungua kesi hiyo, kwa mujibu wa
Kifungu cha 111 (3) cha Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Katika uamuzi uliosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra
Maruma, mahakama hiyo ilirejea kifungu na kusema mtu anayefungua kesi ya
uchaguzi, ni lazima awasilishe maombi ili Mahakama impangie kiwango cha
amana anachopaswa kulipa ndani ya siku 14 tangu kufungua kesi na kwamba
ndani ya siku 14 nyingine tangu siku ya maombi hayo, Mahakama hiyo iwe
imeshapanga kiwango hicho.
Jopo hilo la majaji likielezea umuhimu wa mwenendo huo, lilisema ni
muhimu kwa sababu kuu mbili, moja ni kuipa nafasi Mahakama kuona kama
maombi yaliwasilishwa ndani ya muda baada ya kesi kufunguliwa na pili ni
kuona kama maombi hayo yaliamuliwa ndani ya muda tangu kuwasilishwa.
Comments