KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuwafuata watani zao Simba ambao wako mkoani Morogoro tangu juzi kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba iliwasili Morogoro ikitokea Iringa baada ya mechi yake dhidi ya Lipuli FC wakati Yanga wametua mkoani humo jana baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City jijini Mbeya.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa timu yao imeweka kambi Morogoro na wanaamini ni mahali sahihi kwa lengo la kuwajenga wachezaji wake kuelekea mchezo huo wa Jumapili.
"Timu iko Morogoro, hali ya hewa na mazingira ya kambi ni rafiki, tunaamini benchi la ufundi litapata kile ilichokihitaji kuelekea mchezo wetu dhidi ya watani zetu," alisema Manara.
Naye Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema kuwa kikosi cha Yanga kilitarajiwa kuwasili Morogoro jana jioni tayari kuanza mazoezi ya kuwavaa watani zao.
"Tunaenda kuweka kambi Morogoro," alisema kwa kifupi meneja huyo.
Timu hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, zitakutana huku kila upande ukiwa na kumbukumbu ya kutoka sare katika mechi ya mzunguko wa kwanza wakati Simba yenye pointi 59 ikiwa kileleni kwa ikifuatiwa na Yanga wenye mechi mbili pungufu ukilinganisha na watani zao.
Simba na Yanga ambazo zilitolewa mapema katika mashindano ya Kombe la FA ambayo bingwa wake ataiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, wanafukuzana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ili kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.
Comments