ILIKUWA Aprili Mosi mwaka huu ukumbini Mlimani City katika usiku wa tuzo za Sinema Zetu zilizoandaliwa na Azam TV.
Watu maarufu walihudhuria; Diamond Platinumz alikuwepo na mzazi mwenzake Hamisa Mobeto. Tanzania’s sweetheart Madam Wema Sepetu alikuwepo na wengine wengi.
Lakini kati ya wote hawa, hakuna aliyetajwa mara nyingi na wale waliopata nafasi ya kushika kinasa sauti, kama Haji Sunday Manara, mkuu wa habari na mwasiliano wa Simba SC.
Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, alimtaja Haji. Hata mshindi wa tuzo ya mchekeshaji bora, Hassan Kitale, pia alimtaja Haji.
Wakati wao wakimtaja Haji, yeye aliitaja Simba. Alipopata nafasi ya kushika kinasa sauti…akawaimbisha watu wimbo maarufu wa ‘THIS IS...SIMBAAA’. Nadhani hata mstaafu wetu, Jakaya aliimba, maana alipojikausha, Haji alimuona na kumtaka aimbe…ukumbi ukalipuka. HUYU NDO HAJI MANARA!
Mtu anayeweza kuliteka tukio kubwa kama lile ambalo kimsingi halikuhusiana kabisa na kazi yake huku akiwaacha wenye shughuli yao kama Idris Sultan wakibaki kulalamika tu, siyo wa kubeza hata kidogo.
OMBWE
Simba SC (hata hasimu wao Yanga SC) ni klabu yenye mashabiki nchi nzima, lakini ina wanachama wachache tu, tenawengi wako Dar es Salaam tu. Wanachama hai wa Simba hawafiki (au kama wanafika basi hawazidi elfu kumi). Unapotokea mkutano mkuu wa klabu, ni nadra sana kupata wanachama elfu mbili.
Miaka na mikaka, idadi ni hiyo hiyo tu, haiongezeki. Hii ni bahati mbaya sana!
Idadi ya wanachama haiongezeki siyo kwa sababu mashabiki wanapungua, la hasha.
Simba (na hata Yanga) zinaongeza mashabiki kila uchao.
Kama kwa siku watazaliwa watoto watano, yawezekana watoto watatu wakaangukia kuwa mashabiki wa moja kati ya hizi timu. Lakini watabaki kuwa mashabiki tu, siyo wanachama, mpaka watazeeka na kufa.
Simba SC (na hata mahasimu wao Yanga) hawana utaratibu wa makusudi wa kuongeza wanachama.
Hao wachache walionao wamekuja wenyewe kwa kuhamasishana mitaani kwao.
Hii si sawa, lazima kuwe na mabadiliko, lazima uwepo utaratibu wa makusudi wa kuongeza wanachama kwa sababu hao ndiyo mtaji wa vilabu.
NAMNA YA KUMTUMIA
Simba wanapaswa kumtumia Haji Manara kuongeza wanachama.
Haji anapaswa kufanya ziara nchi nzima kuhamasisha uanzishwaji wa matawi ya wanachama.
Kugawa kadi kwa wanachama wapya na kuhamasisha wanachama wenye kadi mfu, kuzifufua kwa kuzilipia.
Tanzania ina mikoa 31 na wilaya 169. Kila wilaya ikipata wanachama 1000 ina maana kwamba Simba inaweza kuzalisha wanachama hai 169,000. Wanachama hawa wakilipa ada ya uanachama ya Sh10,000 kwa mwezi ina maana kwamba Simba itaingiza Sh169,000,000 kwa mwezi.
Hayo ni makadirio ya chini. Kama wilaya zaitakuwa na wanachama hai zaidi ya 1000 maana yake Simba itavuna mapesa mengi zaidi.
Mvuto wa Haji Manara unapaswa uwe na manufaa kwa Simba. Haji ana mvuto.
Haji ana nyota. Haji ana uwezo wa kujenga hoja.
Haji anaijua Simba ya juzi, jana na ya leo na wapenzi wa Simba wanamkubali sana Haji.
Nasikitika kusema kwamba sauti ya Haji Manara inawavutia mashabiki wengi wa kawaida wa klabu ya Simba na kuiona kama ndiyo sauti rasmi ya klabu kuliko hata sauti ya kaimu Rais, Salim Abdallah ‘Try Again’. Mashabiki wengi wa kawaida wa Simba hawaijui sauti ya Try Again…wanaijua ya Haji Manara.
Bahati mbaya ni kwamba, Simba wanaye mtu wa aina hii lakini hawajui kumtumia. Siku hizi wamemkataza kuropoka (nawaunga mkono) hivyo amejikuta ana nguvu nyingi lakini hana pakuzitumia, anaishia kupambana kupitia mitandao ya kijamii tu.
Yusuph Manji, wakati fulani alipokuwa mwenyekiti wa Yanga, alimteua Sekioni David “Seki” kuwa mwenyekiti wa kamati ya uongezaji wanachama.
Hata hivyo, kamati hiyo haikufanikiwa sana kwa sababu Seki siyo Haji Manara.
Seki hakuwa na muunganiko na Yanga, kabla hajateuliwa hakuna aliyekuwa akijua kwamba yeye ni Yanga. Alipoteuliwa, hawakumuona kama mwenzao. Yawezekana Seki alikuwa na mapenzi na Yanga lakini hakuwa na ‘passion’ nayo. Yawezekana wapo waliojua kwamba Seki ni Yanga mwenzao lakini hakuwa na ‘bond’ nao. Asingeweza kufanikiwa.
Simba wote wanajua kwamba Haji ni mwenzao kwa hiyo muunganiko tayari upo. Wote wanajua kwamba Haji ana ‘passion’ na Simba na anayo ‘bond’.
MFANO RAHISI
Marekani, ambako biashara ya michezo iko juu zaidi ya nchi yoyote duniani, wanawatumia watu wenye mvuto kama wa Haji Manara kutangaza ‘brand’ zao za michezo.
Bilionea Marcelo Claure alipotaka kuanzisha timu yake ya Miami United, alimuita David Beckham na kumfanya kuwa mmiliki mwenza.
Claure alijua kwamba Beckham ana mvuto wa hali ya juu sana hivyo kumshirikisha kwenye timu yake kutavutia ‘attention’ ya watu.
Beckham hakwenda Miami United na mtaji wa hela bali umaarufu wa jina lake.
Na kweli, kila mtu anajua David Beckham anamiliki timu Marekani…lengo limefanikiwa.
Mwaka 2017, mabilionea Berke Bakay na Kona Grill waliinunua timu ya Arizona United SC kutoka kwa Kyle Eng, wakaibadilisha jina na kuiita Phoenix Rising FC. Katika kuifanya timu hii itangazike, wakamsajili Didier Drogba kama mchezaji lakini pia kama mmoja wa wamiliki. Siyo kwamba Drogba alitoa fedha zake kununua hisa, hapana.
Alitoa umaarufu wa jina lake katika kuikuza ‘brand’.
Mvuto wa David Beckham na wa Didier Drogba, ndiyo uliowavutia mabilionea wale kuwaita na kuwafanya wawe wamiliki wenza kwenye timu zao ili watembelee nyota.
Haji Manara kwa hapa kwetu anao umaarufu huo. Haji anao mvuto huo. Haji anaweza kutumika kama taa ya kuing’arisha Simba kubwa na ya kihistoria ya Simba na kufika mbali zaidi.
Viongozi wa Simba wasijidanganye tu kwa kusema kwamba ‘Simba ilikuwa na jina kabla ya Haji’, ni kweli lakini hiyo haimaanishi kwamba haitakiwi kutangazwa zaidi.
Kwa nafasi yake ameweza kuitangaza Simba na wanaweza kumtumia kuendelea kuitangaza Simba.
Credit- Mwanaspot
Comments