SIKU chache kabla ya mchezo wa watani wa jadi, winga wa Simba, Shiza
Kichuya, amepewa darasa la nguvu na Mtanzania anayecheza soka la kulipwa
nchini Ubelgiji, Mbwana Samatta, ambalo linaweza kuleta ‘msiba’ kwa
mashabiki wa Yanga wakati timu zao zitakapokutana Aprili 29, mwaka huu,
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaweza kutoa picha ya ubingwa,
kwani timu itakayoshinda itakuwa na nafasi kubwa kutwaa taji hilo.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kichuya, aliyekuwa miongoni mwa
wachezaji walioichezea timu ya Taifa, Taifa Stars, mchezo wa kirafiki wa
kimataifa dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), alisema
kuwa, baada ya kipute hicho, alifanya mazungumzo ya nguvu na Samatta,
anayekipiga katika klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji.
Kichuya alisema mbali ya kupongezwa na Samatta kutokana na kiwango
alichokionyesha katika mchezo huo, pia alitakiwa na mwenzake huyo
kuongeza juhudi na heshima kwa makocha ili atimize malengo aliyojiwekea.
“Alitaka kujua mipango yangu katika soka, nilipomueleza, aliniambia
niongeze juhudi uwanjani na heshima katika benchi la ufundi, kwani
tayari nimeshaonyesha nina muda mfupi wa kuwapo Tanzania.
“Sitaweza kuweka kila kitu nilichozungumza naye, kwani mengine natakiwa
kuyafanyia kazi, nimemuahidi kuyafanyia kazi yote aliyoniambia, yeye ni
mkubwa kiumri, amenitangulia kucheza na pia ana mafanikio zaidi yangu,
hivyo ushauri wake nitaufanyia kazi,” alisema.
Kutokana na ‘sumu’ aliyopewa na Samatta, Kichuya anaweza kucharuka kwa
kufanya mazoezi kwa bidii mno, hali inayoweza kuziponza timu
atakazokutana nazo hivi karibuni, ikiwamo Yanga.
Kichuya amekuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba wanaoogopewa na timu
pinzani, kutokana na cheche zake awapo uwanjani, zaidi ikiwa ni chenga,
umahiri wake wa kupiga pasi na krosi murua za mabao, lakini pia kufunga.
Winga huyo timu yake ya Simba inapokutana na Yanga, amekuwa akiwaliza
mara kwa mara watani wao hao wa jadi, tena akifunga mabao ya kiufundi
mno.
Comments