Mkataba mabadiliko ya tabia nchi nchi itanufaika kwa kupata fedha za kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi
BUNGE limeridhia makubaliano ya Paris kuhusu kuboresha utekelezaji wa mkataba wa makubaliano ya tabia nchi ambayo pamoja na masuala mengine, nchi itanufaika kwa kupata fedha za kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Kupitia azimio la bunge la kuridhia makubaliano lililowasilishwa jana bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, fedha hizo kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania, zitapatikana kupitia ufadhili wa mifuko ya mabadiliko ya tabia nchi na wadau wengine. “Nchi zilizoendelea zitatakiwa kutoa taarifa kila baada ya miaka miwili kuhusu kiwango cha fedha walizotoa au wanatarajia kutoa kama msaada kwa nchi ambazo ziko hatarini kuathirika na mabadiliko ya tabia nchi,” alisema Makamba.
Waziri Makamba alisema, kwa kuwa Tanzania inaingia kwenye uchumi wa viwanda, makubaliano hayo ya Paris yatasaidia kuchochea matumizi ya gesi asilia, upatikanaji wa teknolojia safi, kufunza wataalamu na kuendelea kuwa na vyanzo vya nishati endelevu kukabiliana na uchafuzi wa mazingira. Wakati huo huo, serikali imesisitiza taasisi za serikali ikiwemo shule, magereza na hospitali kuhakikisha wanaondokana na matumizi ya kuni na mkaa badala yake wanajikita katika nishati ya kupikia isiyo na athari kwa mazingira.
Kwa mujibu wa Waziri Makamba, taasisi zote zimepewa mwaka mmoja na kuagiza kuwa mtu yeyote anayetaka zabuni ya kupika chakula katika taasisi yoyote, ajipange kutotumia mkaa na kuni. Aidha waziri alisema upandaji miti utapewa msukumo mpya na wanatarajia kufanya sensa kubaini miti iliyopandwa. Katika hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni katika Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Ally Saleh Ally, kabla ya azimio hilo kupitishwa na wabunge, alishauri serikali kutenga fedha kutoka vyanzo vya ndani kukabili athari za mabadiliko ya tabia nchi. Kwa upande wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Makamu Mwenyekiti, Innocent Bashungwa alitaja faida zitakazopatikana kutokana na kuridhiwa kwa makubaliano hayo kuwa ni kuwezesha kupambana na changamoto za mabadiliko ya tabia nchi ikiwemo ukame na mafuriko.
Athari nyingine ni kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, kumezwa kwa visiwa vidogo kwenye bahari na maziwa, kuongezeka kwa ujazo wa maji, kuyeyuka kwa barafu katika kilele cha mlima Kilimanjaro na uharibifu wa miundombinu ya barabara na makazi kutokana na mafuriko. Licha ya kipengele cha upatikanaji wa fedha za utekelezaji, vipengele vingine muhimu vya makubaliano hayo ya Paris yaliyopitishwa katika bunge hili la 11 ni pamoja na vinavyotaka kila nchi mwanachama kutunza misitu inayonyonya gesijoto na kila nchi mwanachama kuwajibika kuandaa na kutekeleza mipango ya kuhimili mabadiliko ya tabia nchi. Vile vile umewekwa mfumo wa nchi zinazoendelea kupata teknolojia, kujengewa uwezo na uelewa katika kushughulikia mabadiliko ya tabia nchi, hali ambayo itaongeza uelewa wa jamii kuhusu hatua za kuchukua kupunguza athari.Source Habarileo.
Comments