Serikali ya Israel imetangaza imefikia makubaliano na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR kuufutilia mbali mpango uliozua utata wa kuwarejesha makwao wahamiaji wa Kiafrika na badala yake kufikia mpango mpya ambao utapelekea wahamiaji hao kupelekwa katika nchi za magharibi.
Wahamiaji 16,250 watapewa hifadhi katika nchi za magharibi ambazo Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amezitaja Canada, Italia na Ujerumani kuwa nchi zitakazowapokea maelfu ya wahamiaji kutoka Israel.Netanyahu mnamo mwezi Januari alitangaza nchi yake itaanza kutekeleza mpango wa kuwaondoa nchini humo wahamiaji walioingia kinyume na sheria ifikapo tarehe mosi Aprili iwapo hawataondoka kwa hiari.
Wahamiaji hao wengi wao kutoka Sudan na Eritrea walitishiwa na kifungo gerezani na kuondolewa kwa lazima kutoka Israel. Mpango huo ulikosolewa vikali na mashirika ya kutetea haki za binadamu na hata baadhi ya Waisrael.
Comments