Viongozi sita wa Upinzani nchini Tanzania wamefikishwa mahakamani kusaini hati za dhamana zao na ili kuachiwa huru.
Viongozi hao wa chama cha CHADEMA, akiwemo mwenyekiti Freeman Mbowe, walishtakiwa kwa uchochezi ,kuleta vurugu na kuandamana mwezi wa Februari mwaka huu.
Mjumbe mwingine , Halima Mdee, ameongezewa kwenye mashtaka na kufanya jumla ya washtakiwa kuwa saba.
Hapo awali,mjumbe wa Chadema, Halima Mdee alikamatwa alfajiri jana, Aprili Mosi katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere akitokea nchini Afrika Kusini inakoeelezwa alilalzwa kwa matibabu.
Kwa mujibu wa ukurasa wa Facebook wa Chadema Media imesema kwamba "Tunatoa mwito kwa Jeshi la Polisi limpatie dhamana ili aweze kuendelea na matibabu yake, Kwani dhamana ni haki yake na zaidi ni kuwa huyu bado ni mtuhumiwa na ni Mgonjwa ambaye ametoka hospitalini."
Eagan Salla, mwandishi wa BBC aliyopo katika mahakama ya Kisutu anasema, 'hali ya ulinzi mahakamani imeimarishwa ijapokuwa wafuasi wa chadema nao wanaonekana nje ya mahakama wakisubiri hatima ya viongozi wao'
Alhamisi iliopita, mahakama ya hakimu mkazi Kisutu iliwapatia dhamana viongozi hao sita lakini kusema kuwa watasalia rumande hadi kesi leo tarehe 3 Aprili ambapo wataletwa mahakamani kukamilisha masharti ya dhamana.
Wanasiasa hao hawakuletwa mahakamani katika uamuzi wa dhamana yao huku afisa wa magereza akiiambia mahakama ni kutokana na gari lililotakiwa kuwasafirisha kuja mahakamani hapo kuwa bovu.
Miongoni mwa mashtaka waliyosomewa ni pamoja na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha NIT Akwilina Akwiline.
Wanashtakiwa pia kuendelea kufanya mkusanyiko usio halali wilayani Kinondoni shtaka linalowakabili washtakiwa wote.
Hatua hii ya viongozi hawa kuendelea kusota rumande wakisubiria dhamana inaleta picha gani?
Akizungumza na BBC, mchambuzi wa maswala ya siasa Rashid Chilumba anaelezea kwamba kampeni ya kuwelenga upinzani katika awamu iliopo imevuka "mstari mwekundu"
"Viongozi wa upinzani wanapowekwa ndani haitoi taswira nzuri katika mwenendo wa siasa ya ushindani, hasa ukizingatia kwamba kume kuwa tayari na wasiwasi kuwa utawala unebana zaidi upinzani" alielezea Chilumba.
Kesi gani zinazowaandama wanasiasa wa upinzani hasa Chadema?
Kwa mujibu wa baadhi ya vyanzo, kuna wabunge 13 wa chama hicho wanaokabiliwa na kesi katika mahakama mbalimbali.Chama kikuu cha upinzani Chadema ndicho kinachoonekana kuwa na idadi kubwa ya wanasiasa wake wanaozongwa na kesi mbali mbali.
Mbunge wa Singida, kupitia chama cha chadema Tundu Lissu ambaye kwa sasa yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu,anakabiliwa na kesi sita. Kesi zote zinahusiana na uchochezi.
Lissu anasemekana kuwa ndiye mwanasiasa aliyekamatwa mara nyingi zaidi ya wengine. Miongoni mwa kesi zake zilizoibua mjadala mkubwa ndani na nje ya nchi ni ile aliyoshutumiwa kutoa matamko ya uchochezi na kumuita Rais John Magufuli 'dikteta uchwara'.
Joseph Mbilinyi, maarufu kwa jina la kazi zake za usanii Sugu, ambaye ni mbunge wa Mbeya mjini, sasa yuko gerezani kwa kipindi cha miezi mitano baada ya mahakama kumkuta na hatia ya kutumia lugha za matusi dhidi ya Rais Magufuli.
Kwa upande wake Halima Mdee, mbunge wa jimbo la Kawe jijini Dar es salaam, yeye anazo kesi nne zote zikiwa za uchochezi ikiwemo ile aliyotuhumiwa kutumia lugha mbaya kumpinga Rais Magufuli baada ya kutangazwa kwa marufuku ya kuwaruhusu wanafunzi wa kike kurudi shuleni mara wapatapo ujauzito.
Mbunge wa Arusha Godbless Lema yeye anakabiliwa na kesi nne pia huku zote zikiwa za uchochezi. Siku za nyuma Lema aliwahi kukaa mahabusu kwa muda wa miezi minne kwa kosa la uchochezi. Hivi sasa Lema amekuwa akihudhuria mahakamani mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Chadema taifa na kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni Freeman Mbowe yeye ana kesi 3 ikiwemo kesi ya wiki hii. Kwa sasa anahitajika kuhudhuria polisi kila siku.
John Mnyika mbunge wa jimbo la ubungo jijini Dar es salaam kwa upande wake anahitajika kuhudhuria polisi kila wiki tangu jaribio la kufanyika kwa maandamano ya chama hicho mwezi uliopita. Huyu kesi yake yeye bado haijawekwa wazi
Mbunge wa Mara, Esther Bulaya, aliwahi kushikiliwa na polisi kwa kosa la kutaka kuandaa mkutano wa hadhara nje ya jimbo lake, jambo ambalo polisi walidai kuwa lilikuwa ni uvunjifu wa sheria.Source BBC
Comments