Serikali inaendelea na mikakati wa kuhakikisha wananchi wake wanapata huduma bora za afya na kwa wakati ili kuleta ustawi katika kufikia azma ya Tanzania ya viwanda.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Mbeya na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Constantine Mushi alipokuwa akizinduzi mafunzo kwa wakufunzi wa kitaifa kuhusu Bima ya Afya ya Jamii (CHF), mfumo wa kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma (DHFF), na mfumo wa manunuzi ya dawa nje ya mfumo wa kawaida wa MSD (Jazia – Prime Vendor System).
Kaimu Katibu Tawala huyo aliongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na afya ya uhakika kwa kupata huduma bora za afya na kwa wakati, jambo lililopelekea kuanzishwa kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja katika vituo vya kutolea huduma tofauti na ilivyokuwa hapo nyuma.
“lengo mahususi ya mafunzo haya ni kuelewa kwa upana maana ya mipango ya afya na bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma (DHFF)”yenye matarajio ya kupunguza urasimu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa kuimarisha uwajibikaji na uboreshaji wa uandaaji wa mipango, bajeti na matumizi yanayolenga kuboresha huduma za afya,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa mpaka sasa katika robo ya pili ya mwaka Serikali imekwisha peleka takribani shilingi bilioni 45 katika jumla ya vituo vya kutolea huduma za afya 5,125 nchi nzima.
Comments