TANZANIA itanufaika kwa kiasi kikubwa kutokana na ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya Mrisho Kikwete nchini Kuwait.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete na Mtawala wa
Dola ya Kuwait Amiri Sabah Al-Ahmad Al-Jaber Al-sabah katika mazungumzo
mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kuwait
City Mei 5, 2013
Manufaa hayo kwa Tanzania yametangazwa katika mazungumzo rasmi na kati
ya Rais Kikwete na Kiongozi wa Kuwait, Emir Sheikh Sabah Al Ahmad Al
Jaber Al Sabah na katika mazungumzo na Naibu Mkurugenzi wa Mfuko wa
Kuwait wa Maendeleo ya Nchi za Kiarabu (Kuwait Fund) Ghanim Sulaiman
Al-Ghaniman.
Katika mazungumzo yaliyofanyika kwenye kasri ya Bayan kabla ya
kumwandalia dhifa ya kitaifa Rais Kikwete, kiongozi wa Kuwait aliahidi
kuwa nchi yake itaisaidia Tanzania katika miradi yote ya maendeleo
ambayo serikali ya Tanzania imeomba kuungwa mkono wakati wa ziara ya
siku mbili ya kiserikali ya Rais Kikwete.
Emir alimwambia Rais Kikwete kuwa nchi yake tayari imetoa fedha za
kufanyia upembuzi yakinifu wa ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahua katika
mikoa ya Singida na Tabora na inafikiria kutoa fedha za ujenzi wa
barabara hiyo yenye kilomita 90 katika kiwango cha lami.
Ujenzi wa kipande hicho cha barabara ni sehemu ya barabara ya kilomita
700 ya kuunganisha Manyoni, mkoa wa Singida na Kigoma na ujenzi wake
utakuwa umekamilisha kwa asilimia kubwa barabara hiyo muhimu kwa
mawasiliano ya kutoka magharibi kwenda mashariki mwa Tanzania.
Comments