Na Abdi Said, Mogadishu
Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, Misheni ya Umoja wa Afrika
nchini Somalia (AMISOM) imefungua kliniki za afya nane na hospitali tatu
katika maeneo yaliyokombolewa kutoka kwa al-Shabaab, kwa mujibu wa
msemaji wa AMISOM Kanali Ali Aden Humad.
Wakina mama na watoto wakisubiri huduma za
matibabu kwenye kituo cha jeshi cha AMISOM huko Halane jijini
Mogadishu. [Abdi Said/Sabahi]
Kliniki hizo zipo katika wilaya kadhaa za mikoa ya Shabelle ya Kati na
ya Chini, na hospitali hizo zipo Beledweyne, Kismayo na Baidoa. Zinatoa
huduma kamili mbalimbali za afya, Humad alisema.
"Tuna vifaa vya kisasa vya huduma za afya, ikiwa ni pamoja na vifaa vya
maabara kwa ajili ya kuchunguza magonjwa ya kawaida, mashine ya kufanya
eksirei kwa jeraha ya mfupa, mashine ya kuchunguza shinikizo juu la damu
na kisukari, na dawa hutolewa bure na madaktari wenye sifa za hali ya
juu," aliiambia Sabahi.
AMISOM imeweka katika hospitali hizo madaktari wawili na wauguzi kumi
kwa kila moja ili kuhudumia wagonjwa wapatao 300 kwa siku. Vituo vidogo
vya afya huhudumia wagonjwa wachache, Humad alisema. Kliniki jongevu za
afya pia zipo na zinatoa huduma vijijini.
Abdi Malim Hussein, mwenye umri wa miaka
12, akipata huduma za matibabu katika hospitali ya AMISOM jijini
Mogadishu. Hussein alipigwa risasi kwenye nyonga mwezi Machi na
al-Shabaab baada ya yeye na marafiki zake wanne kujaribu kutoroka kwenye
kambi ya mafunzo katika wilaya ya Mahadey huko Shabelle ya Kati mahali
walipopelekwa na kushikiliwa mateka. [Abdi Said/Sabahi]
AMISOM ilifungua vituo hivyo baada ya kushauriana na wazee wa kimila,
ambao waliwaambia kwamba huduma za afya miongoni mwa watu zinahitajika
sana. Gharama za uendeshaji zinatoka moja kwa moja kwenye bajeti ya
AMISOM.
Comments