Mwanza. Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema
wakati ukifika, yeye na rafiki zake Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Kimataifa, Bernard Membe, Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe, watachagua mmoja wao
watakayeona anafaa kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Samweli sitta
Waziri Sitta aliyasema hayo jana katika Kongamamo la Mawasiliano katika
Nyanja za Digitali la wanafunzi wa Idara ya Uhusiano na Masoko, Chuo
Kikuu cha St. Augustine (SAUT), Mwanza.
Mara ya kwanza, Sitta aliwataja rafiki zake hao juzi wakati wa harambee
ya kuchangia Kanisa Katoliki, Josephine Bakita, Parokia ya Igoma,
Mwanza.
Pia alisema hatagombea tena Ubunge Urambo ya Mashariki baada ya kuwa
katika ulingo wa siasa kwa miaka 35 na badala yake ataangalia namna
nyingine ya kuwatumikia wananchi huku akigusia mchakato wa kuwania urais
ambao, alisema anamwachia Mungu.
“Kwa ubunge nimekwisha waeleza inatosha sitagombea tena kwani miaka 35
inatosha, … lakini hatima yangu ni nini siwezi kujua lakini nina afya
nzuri na mmoja wa wanasiasa wakongwe, wenye afya nzuri, mnaona
ninavyopendeza... kwa urais namwachia Mungu tutaona,” alisema Sitta.
Alisema yeye rafiki zake hao wana mawazo yanayolingana katika
mustakabali wa nchi hii na kwamba wataendelea kutembea sehemu mbalimbali
za nchi kuwajengea wananchi uelewa ili wajue kuwa uongozi ni lazima
ukae katika mikono salama.
Comments