Umoja wa Mataifa umesema kuwa, una wasi wasi wa kuzuka tena machafuko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa, vikosi vya kusimamia amani
vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeelezea
wasi wasi wake wa kuanza tena mapigano baina ya vikosi vya serikali na
waasi wa M23 jirani na mji wa Goma mashariki mwa nchi hiyo.
Eduardo del Buey, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa
amewaambia waandishi wa habari kwamba, kumezuka mapigano katika maeneo
ya Kibati na Rusayo yapata kilomita 12 kutoka katika mji wa Goma baina
ya wapiganaji wa waasi wa M23 na vikosi vya serikali ya Kinshasa.
Eduardo del Buey ameongeza kuwa, vikosi vya kusimamia amani vya Umoja
wa Mataifa vilivyoko Congo DRC vimeripoti kwamba, pande mbili zilitumia
silaha nzito katika mapigano hayo.
Katika upande mwingine, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
imepanga kujenga bwawa litakalokuwa kubwa zaidi duniani itakapofika
mwaka 2015.
Taarifa zinasema kuwa, bwawa hilo lilikuwa lijengwe miaka kadhaa
iliyopita, lakini ilishindikana kutokana na ukosefu wa fedha za
kugharamia ujenzi huo.
Chanzo - kiswahili.irib.ir
Comments