Na Hassan Hamad OMKR
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad,
amewahimiza wazazi, walezi na walimu kushirikiana kutika kurejesha
maadili na malezi bora kwa watoto.
Maalim Seif ametoa wito huo wakati akizungumza katika hafla ya maulid ya
Mtume Muhammad (SAW), yaliyoandaliwa na Madrasat Ghulam Islamia ya
Muembe Makumbi mjini Zanzibar.
Amesema maadili ya kiislamu na malezi bora kwa watoto yanaweza
kurejeshwa iwapo jamii itakubali kushirikiana katika malezi, sambamba na
kushajiisha elimu ya madrasa kwa vijana.
“Sisi wakati wetu mtoto alikuwa akilelewa na jamii nzima, yaani kama
mtoto akikosea au kuondosha nidhamu na heshima kwa mzee mwengine basi
alikuwa na uwezo wa kumrudi mtoto yule, na akienda kushtaki kwao basi
mzazi wake atamuongeza kutokana na kosa hilo, lakini leo wapi, mambo
yamebadilika”, alieleza Maalim Seif huku akitoa historia ya malezi ya
zamani.
Aidha amesifu juhudi za walimu wa madrasa katika kuwaendeleza watoto
kitaaluma, licha ya kukabiliwa na mazingira magumu, na kuwataka walimu
hao kujipanga katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili ikiwemo
ukosefu wa mishahara.
Comments