Na Mwandishi Wetu
Tume ya Mabadiliko ya Katiba imesema haimzuii mwananchi, asasi au
taasisi yoyote kufungua kesi Mahakamani kupinga au kuzuia mchakato
unaoendelea wa Katiba Mpya.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba ametoa ufafanuzi huo kwa
baadhi ya waandishi wa habari waliofika ofisini kwake jijini Dar es
Salaam leo (Jumatano, Mei 15, 2013) kutaka ufafanuzi wa masuala
mbalimbali yaliyotolewa na Jukwaa la Katiba jijini Dar es Salaam jana
(Jumanne, Mei 14, 2013).
Katika tamko lake, Jukwaa la Katiba lilieleza nia ya asasi yake kufungua
kesi Mahakama Kuu ya Tanzania ndani ya siku saba ili kusimamisha
mchakato wa katiba Mpya kutokana kile ilichodai ni kasoro zinazojitokeza
katika mchakato wa katiba unaoendelea.
Ruksa kwenda Mahakamani
Hata hivyo, akiongea na baadhi ya waandishi wa habari waliofika leo
ofisini kwake leo, Jaji Warioba alisema Tume yake haina tatizo na mtu au
asasi kwenda Mahakamani kwa kuwa hiyo ni haki yao ya kikatiba.
“Nimesoma tamko lao na niseme tu halina jipya. Hii si mara ya kwanza
kusikia hili (la kwenda Mahakamani), na jibu letu lilikuwa waende na
ndio jibu letu hadi sasa,” alisema Jaji Warioba anayeongoza Tume hiyo
iliyoanza kazi Mei 2 mwaka jana.
“Mimi nasema waende ili tujue Jukwaa haswa ni nani, kwa sababu
ninafahamu ni mkusanyiko wa asasi mbalimbali na baadhi ya asasi hizohizo
zimetuletea maombi ya kuunda Mabaraza ya Katiba ya Taasisi na Asasi…
sasa jukwaa hili ni nani haswa?,” alisema Jaji Warioba.
Comments