MWENENDO wa Bunge la Bajeti linaloendelea mjini hapa, umebaini kuwa vita
ya maneno, fitna kati ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), sasa imehamia bungeni, Tanzania Daima
Jumatano limebaini.
Moto wa vita hiyo kati ya vyama hivyo hasimu, umekolezwa zaidi baada ya
Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete kufanya mkutano wa
kimkakati na wabunge wa chama chake mjini hapa.
Duru za siasa kutoka ndani ya kikao hicho cha wabunge na rais, zilieleza
kuwa Rais Kikwete aliwataka wabunge hao wa CCM wajipange kukabiliana na
hoja za CHADEMA ambazo katika siku za hivi karibuni zimeonekana
kulitikisa Bunge kiasi cha kiti cha spika kuamua kutumia kanuni
kandamizi kuzizima.
Wabunge wa CCM bila kujali uzito wa hoja, wameamua kukabiliana na hoja
zozote za wabunge wa CHADEMA hata kama zina maslahi kwa taifa.
Tayari CHADEMA kimeeleza kubaini mbinu hizo, kikidai kuwa hata kitendo
cha Spika Anne Makinda kukatisha hotuba ya msemaji wao katika Wizara ya
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Joseph Mbilinyi ilikuwa sehemu ya
utekelezaji wa mkakati huo.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema kuwa
hatua hiyo ndiyo iliwafanya wasikubali kubadili hotuba yao hiyo kuanzia
ukurasa wa kwanza hadi wa 14 kama ilivyotakiwa na spika kwani ni kinyume
na kanuni ya 63 (2).
Comments