Baada ya kushinda ubingwa wa ligi ya Ujerumani, Bundesliga, kabla ya
ligi hiyo kufikia mwisho na kuweka rekodi ya aina yake ya pointi, sasa
Bayern Munich imetia kibindoni taji lake la tano la ubingwa wa Ulaya.
Ni Arjen Robben ndiye aliyepachika bao la ushindi katika dakika ya 89 na
kuipatia Bayern Munich ushindi muhimu dhidi ya mahasimu wao Borussia
Dortmund jana Jumamosi (25.05.2013), baada ya mchezo wa kuvutia wa
fainali ya ChampionsLeague katika uwanja wa Wembley mjini London.
Wakati muda wa nyongeza ukipiga hodi, Robben alipokea pasi ya kisigino
kutoka kwa Frank Ribery, akamkwepa Mats Hummels na kuuweka mpira wavuni
akimwacha Roman Weidenfeller bila majibu na kuipatia Bayern Munich taji
lake la tano la mabingwa wa Ulaya.
Ulikuwa muda uliokuwa unasubiriwa mno kwa Bayern na Robben baada ya
kushindwa kulitwaa taji hilo katika fainali za mwaka 2010 na 2012,
wakati walipobwagwa kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Chelsea London
katika uwanja wake wa nyumbani.
"Kipindi changu chote cha kucheza soka kilipita katika mawazo yangu
wakati nilipopachika bao hilo. Ni hali ya kipekee kabisa unayoweza
kuihisi, huwezi kuielezea," Robben amesema.
Heynckes amwagiwa sifa
Kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, akifurahia ushindi.
Lakini zaidi ni kocha wa Bayern Munich, Jupp Heynckes, ambaye
alimiminiwa sifa tele baada ya timu yake kunyakua taji hilo. Rais wa
klabu hiyo, Uli Hoeness, alimwagia sifa Heynckes mwenye umri wa miaka 68
ambaye anaweza kushinda mataji matatu na Bayern mwishoni mwa juma
lijalo iwapo timu hiyo itaishinda VFB Stuttgart katika fainali ya Kombe
la Shirikisho, DFB Pokal.
"Nimefurahi kwamba klabu hii sasa iko juu kabisa katika Ulaya," Hoeness amesema.
"Jupp amefanya kazi nzuri sana. Kuiweka timu hii na nyota wake wote
katika hali sahihi na kuifanya kuendelea kufanya vizuri katika kiwango
cha juu kabisa ni mkono wa Jupp Heynckes."
Mchezaji wa kiungo wa Bayern Munich, Bastian Schweinsteiger, amesema:
"Tumekuwa na msimu mzuri sana na Heynckes ana sehemu kubwa katika
mafanikio hayo. Anakwenda na wakati na anaongoza akiwa mbele."
Comments