Wahisani waahidi Dola milioni 600 kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali kukabiliana na magaidi
Mkutano wa Kimataifa uliowaleta pamoja Viongozi wa nchi za Afrika na
Maofisa wa Kimataifa umefanikiwa kukusanya jumla ya dola milioni 600 kwa
ajili kusaidia vita vinavyoendelea Kaskazini mwa Mali.
Wanajeshi wa Ufaransa wakiwa katika Mji wa
Timbuktu baada ya kuuchukua kutoka kwa Makundi ya Kiislam.
REUTERS/Arnaud Roine/ECPAD/Handout
Wafadhili mbalimbali wamechangia fedha kwa ajili ya kuendeleza vita
iliyopewa jina Vita ya Kupambana na Ugaidi Kaskazini mwa Mali lengo
likiwa ni kuyasambaratisha Makundi ya Kiislam yaliyokuwa yanatawala kwa
miezi zaidi ya tisa.
Mkutano huo umefanyika nchini Ethiopia ambapo mataifa hayo yameahidi pia
kuchangia kijeshi ili kufanikisha kukabiliana na vitendo vya kigaidi
ambavyo vyanzo vyake vimekuwa vikitanjwa kuwa nchini Mali.
Japan imechangia dola milioni 120 huku Marekani ikitoa kitita cha dola
milioni 96 kati ya dola milioni 600 ambazo zimeahidiwa kutoka kwa nchi
ambazo zimehudhuria mkutano huo maalum wa kuchangisha fedha.
Mkutano huo umehudhuriwa na Wawakilishi kutoka Umoja wa Mataifa UN,
Umoja wa Ulaya EU na China ambao wote wameahidi kutoa fedha kwa ajili ya
kusaidia operesheni hiyo ya kijeshi.
Rais wa Mali Dioncounda Traore ameishukuru Jumuiya ya Kimataifa kwa
mchango ambao wameutoa kwa nchi hiyo katika na kuahidi watakuwa tayari
kutoa ushirikiano wa hali na mali.
Umoja wa Afrika AU umeahidi kutoa dola milioni 50 kusaidia operesheni
hiyo ya kijeshi huko Kaskazini mwa Mali ambayo imekadiriwa kugharimu
dola milioni 460 ili iweze kukamilika.
Comments