MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, imetoa masharti ya dhamana kwa msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, ambaye anakabiliwa na kesi ya kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Hata hivyo, Lulu ambaye alikuwa na uso wa furaha jana baada ya kutolewa kwa masharti hayo, alirudishwa rumande kutokana na kutokuwepo kwa Msajili wa Mahakama Kuu wa kanda hiyo, kwa ajili ya kuhakiki iwapo masharti yaliyotolewa na Jaji Zainabu Mruke yametimizwa.
Masharti hayo ya dhamana ni kwamba, muombaji (Lulu) awasilishe hati zake zote za kusafiria kwa Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, asisafiri nje ya mkoa wa Dar es Salaam bila ya idhini ya msajili, kuripoti kwa msajili kila tarehe moja ya kila mwezi tangu atakapotimiza masharti hadi shauri litakapomalizika.
Masharti mengine ni Lulu awe na wadhamini wawili watakaotia saini bondi ya sh. milioni 20 kila mmoja na wawe wafanyakazi wa serikali na Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, atahakiki masharti hayo ya dhamana kama yametimizwa.Inatoka kwa mdau.
Comments