Na Ratifa Baranyikwa
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana
katika kikao maalumu kutafakari na kupanga mikakati katika mambo makuu
manne, likiwamo la Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2014/2015.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam katika
Hoteli ya Blue Pearl, ambako kikao hicho kinaendelea leo, Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema wameamua kujifungia na
kupanga mikakati ya Uchaguzi wa Serikali na Mitaa mwaka 2014 na ule
Mkuu wa mwaka 2015 ili kujiweka sawa.
Hatua hiyo ya CHADEMA imekuja wakati ambapo vita ya urais imeendelea
kushamiri ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku vigogo wanaotajwa
kuwania nafasi hiyo nao wakionekana kujipanga na kuandaa mikakati
kuelekea mwaka 2015.
CHADEMA kinaonekana kuwa ndicho chama pekee cha upinzani ambacho
kimejizolea umaarufu mkubwa kwenye medani ya siasa katika miaka ya hivi
karibuni, kikichukua nafasi iliyokuwa imekaliwa na Chama cha Wananchi
(CUF), hivyo kuonekana kuwa tishio dhidi ya chama tawala.
Upepo wa CHADEMA ulionekana kuvuma vema wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2010 ambapo kilishika nafasi ya pili nyuma ya CCM, hali ambayo
imesababisha macho na masikio mara zote kuelekezwa kwenye chama hicho
kikuu cha upinzani, hasa linapokuja suala zima la kuangalia jinsi
kilivyojipanga kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika mkutano huo wa jana na wanahabari, Mnyika alisema kikao hicho cha
siku mbili ambacho kinamalizika leo kimekuwa maalumu kwa sababu ya
unyeti wake, lakini pia kimeshirikisha wabunge wa chama hicho na kuahidi
kueleza namna uamuzi utakavyofikiwa mara baada ya kikao hicho.
Comments