NA RAMADHANI ALI /MAELEZO 8.1.2013
Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema Zanzibar ni miongoni mwa nchi chache Duniani zinazoendelea kutoa Elimu bila malipo tokea kuasisiwa Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Akizungumza katika ufunguzi wa Skuli mpya ya Sekondari ya Mapinduzi, Chaani katika maadhimisho ya sherehe za kutimiza miaka 49 ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mzee Mwinyi amesema mafanikio hayo yanatokana na viongozi shupavu wa Mapinduzi na wale waliofuatia kuongoza Zanzibar.
Amewapongeza viongozi na wananchi wa
Zanzibar kwa jumla kwa kuendeleza malengo ya Mapinduzi ya 1964 ya
kuimarisha maendeleo katika nyanja mbali mbali.
Rais mstaafu amewahimiza wananchi kuendeleza Umoja kwani bila umoja na mshikamano hakuna maendeleo yatakayopatikana.
Amewashukuru wahisani wanaosaidia
maendeleo ya Zanzibar hasa katika nyanja ya elimu na afya na amesema
misaada yao itaendelea kuthaminiwa .
Amewataka wazee wa Chaani kuendelea
kuwasimamia watoto wao na kuhakikisha wanaitumia skuli hiyo katika
kubadilisha uwezo wao wa kusoma kuwa bora zaidi.
Akizungumza katika sherehe hiyo,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Ali Juma Shamhuna amesema baada ya
kupata msaada wa skuli mpya 19 za sekondari na Benki ya Dunia na skuli
mbili msaada wa BADEA, Wizara yake inatilia mkazo katika kuondosha
tatizo la walimu wa sayansi linalokabili Skuli nyingi za Zanzibar.
Amesema Nigeria imewapatia msaada wa
walimu 13 wa sayansi na tayari wamefanya mazungumzo na nchi ya Marekani,
Uingereza, Ghana, India, Palestina, Misri na Oman na wote wameonyesha
azma ya kusaidia kupunguza tatizo hilo.
Ameongeza kuwa Chuo Kikuu cha Taifa
Zanzibar (SUZA) kwa kuliona tatizo la walimu wa sayansi, kimeanzisha
Skuli ya Sekondari ya sayansi na Chuo cha Ufundi Karume kimeimarisha
somo la hesabu na ameeleza matarajio yake kwamba baada ya miaka mitatu
tatizo hilo litapungua.
Waziri Shamhuna ameahidi Wizara yake
itawaajiri wahitimu wote wa digrii ya sayansi na kuwapa mafunzo ya
ziada walimu wa sayansi ambao wameajiriwa ili kukabiliana na changamoto
hiyo.
Skuli ya Sekondari ya Mapinduzi,
Chaani imegharimu shilingi bilioni 1.32 na imejengwa na kampuni ya
Chaina Railway Jian Chang Engineering Co. LTD ya
China.
IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO
Comments