SEHEMU YA MAONI ALIYOYATOA MH. EDWARD LOWASSA
Kwanza ningependa kukupongeza wewe mwenyekiti Mh Jaji Warioba pamoja na
tume nzima kwa imani kubwa ambayo Rais ameionesha kwenu, ni kwa kuwapa
jukumu hilo zito na muhimu kwa nchi yetu.
Januari 22, 2013: Aliyewahi kuwa Waziri
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Edward Lowassa, akiwasilisha maoni yake kwa
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko katika ofisi za Tume hiyo leo Jijini Dar
es Salaam. (picha: Tume ya Mabadiliko ya Katiba)
Wananchi pia wamekuwa na imani kubwa na wamejenga matumaini ya kila kitu
kwa tume hii. Kutokana na hilo wamekuwa wakitoa maoni ambayo mengine
hayahusiani na katiba, yaani siyo ya kikatiba.Pengine na mimi nitakuwa
miongoni mwao, kwa hiyo naomba radhi mapema, iwapo maoni yangu haya
mengine , yataonekana si ya kikatiba.
Katiba yetu ya sasa ni nzuri, imetuongoza katika umoja na mshikamano wa
kitaifa kwa muda wote huo.Lakini, kutokana na hali ya dunia ya sasa, ni
vyema kuwepo na katiba mpya ili kuendana na hali halisi.
Kuna mambo manne ambayo kwa imani na mtizamo wangu ningependa yawemo katika katiba yetu ijayo.
1.ELIMU BURE
Moja ya haki za mtoto ni kupata elimu. Ningependa suala la elimu bure ya
sekondari liwemo kwenye katiba yetu. Katiba itamke wazi kuwa elimu ya
sekondari ni bure.Nchi yetu bado ina idadi kubwa ya watu wake ambao ni
masikini.
Uwezo wao wa kipato ni mdogo.Naamini kabisa hili linawezekana na
serikali inaweza kugharimia elimu ya sekondari ikawa bure. Hii itatoa
nafasi ya kujenga taifa lijalo lenye idadi kubwa ya vijana watakaokuwa
wamepata elimu ya sekondari.Wabunge wenzangu bila shaka wanalijua hili.
Ukweli katika majimbo yetu wazazi wamekuwa wakishindwa kulipia karo ya
shule kwa watoto wao. Wabunge tumekuwa tukibeba mzigo huo japo kidogo.
Kwa hiyo, kifungu cha ELIMU BURE KWA SEKONDARI, kiwepo kwenye katiba.
2.ADHABU YA KIFO-DEATH PENALT
Katiba ya sasa haisemi wazi kuhusu adhabu ya kifo.Inazungumzia tu haki
ya uhai.Ibara ya 14 ya katiba hii ya jamuhuri ya muungano wa tanzania ya
mwaka 1977 inatamka kiujumla tu kuwa KILA MTU ANA HAKI YA KUISHI NA
UHAI WAKE KULINDWA.
Lakini , haki hiyo inanyang'anywa na kifungu nambari 196 cha sheria ya
kanuni za adhabu sura ya 16(penal code ,cap 16), kinachotamka kuwa
adhabu ya kifo(death penalty or capital punishment) kwa kosa la mauaji
ya kukusudia.
Adhabu hiyo hiyo pia utolewa kwa kosa la uhaini.Sasa mapendekezo yangu
mimi ni kwamba kuwe na ibara katika katiba mpya inayotamka wazi kuwa
HAKUTAKUWA NA ADHABU YA KIFO HAPA NCHINI HATA KWA KOSA LA KUKUSUDIA AU
UHAINI.
3.MATUMIZI YA FEDHA KATIKA UCHAGUZI
Katika sehemu nyingi hapa nchini mwananchi kama hana fedha hawezi
kugombea nafasi mbalimbali za uongozi.Katiba mpya iwe na ibara
inayofafanua ni kiasi gani cha fedha ambacho mgombea anaruhusiwa kutumia
katika kampeni. Iainishe ni matumizi gani ya lazima ambayo mgombea
hawezi kukwepa kutumia fedha katika kampeni zake, mfano kuwakusanya
wapiga kura kwenda kupiga kura gharama hizo nani azibebe.
Katiba ifafanue rushwa ni nini kwenye chaguzi hizi.Au tuwe na mfumo wa
PROPORTIONAL REPRESENTATION ,vyama viwe ndiyo vinaingia kwenye chaguzi
kuwania majimbo na siyo wanachama,huko kila mtu atakuwa anapigania chama
chake kupata kura nyingi ili wapate viti vingi zaidi, pengine hii
itasaidia kuondoa kikwazo cha mtu kuwa na uwezo wa kifedha ndiyo aweze
kuwania uongozi.
4.ARDHI
Kwa mwanadamu, kunyang'anywa haki ya kutumia ardhi ya nchi aliyozaliwa
ni sawa na kunyanng'anywa haki ya uraia wake. Katiba hii ya sasa inawapa
nguvu wakulima katika suala la ardhi, na kuwasahau wafugaji.
Wafugaji wamekuwa wakimbizi katika nchi yao, wamekuwa wakitangatanga
kutafuta malisho ya mifugo yao, ile ardhi waliyokuwa wanaimiliki
wakiondoka kutafuta malisho huku nyuma imekuwa ikimilikishwa watu
wengine, wakulima au wawekezaji, hili kwakweli si jambo jema .
Tumeshuhudia migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.Kwa hiyo,
mimi ningependa katiba hii mpya impe mfugaji haki katika suala la ardhi
kama.Ardhi ya wafugaji ilindwe, ifafanuliwe kikatiba haki yao hiyo. Kuwe
na hali ya 50,50 situation kati ya mfugaji na mkulima katika suala zima
la umiliki wa ardhi, kikatiba!
Chanzo: michuzijr.blogspot.com
Comments