Taasisi
na mataifa mbalimbali duniani yamepinga hotuba ya Rais Bashar al-Assad
wa Syria aliyoitoa Jumapili (6.1.2013) na kusema ni lazima angátuke ili
kumaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea nchini mwake.
Katika hotuba hiyo Rais al-Assad amefuta uwezekano wa kuwa na mazungumzo
na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa ni "vibaraka" wa mataifa ya
magharibi na ameapa kuendelea kupambana na "magaidi" na "magenge ya
wahuni " wanaotaka kuangusha utawala wake.
Akizungumza katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya kipindi cha
zaidi ya miezi saba, Rais Assad amewaita wapinzani wake kuwa ni maadui
wa wananchi na maadui wa Mungu ambao wameamua kufanya ugaidi.
Tunapambana na magaidi: Assad
Assad ameongeza kusema kwamba wapinzani wanaziita harakati zao kuwa ni
mapinduzi lakini kumbe wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi.
"Haya sio mageuzi kwasababu mageuzi kwa kawaida ni harakati za watu na
sio vita vya wageni dhidi ya watu. Mapinduzi ni kusimama kwa ajili ya
watu na sio dhidi ya watu. Hawa si wanamapinduzi, hawa ni baadhi tu ya
wahalifu wa kawaida", alisema Assad.
Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza
mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe
huku wakisema "Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad."
Katika hotuba hiyo Rais Assad alitaja mpango wa kumaliza vita
vinavyoendelea nchini mwake ambao unajumuisha kufanyika kwa mjadala wa
kitaifa wa mazungumzo ya amani, chaguzi za bunge na kuandikwa katiba
mpya.
Comments