NA FURAHA OMARY WA GAZETI LA UHURU
“WATU waendelee kuniombea, hii ni dhamana tu, lakini kesi bado, safari ni ndefu. Namshukuru Mungu, yeye ndiye kila kitu.”
Hiyo ni kauli ilitolewa na msanii wa maigizo nchini, Elizabeth Michael ‘Lulu’, baada ya kuachiwa kwa dhamana na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi inayomkabili ya kuua bila kukusudia.
Lulu, ambaye alikuwa anasota rumande kwa takriban miezi minane katika gereza la Segerea, kuanzia Aprili mwaka jana, anashitakiwa kwa kumuua bila kukusudia msanii mwenzake, Steven Kanumba.
Msanii huyo aliachiwa huru kwa dhamana jana na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu wa Kanda hiyo, Francis Kabwe baada ya kutimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa juzi na Jaji Zainabu Mruke wa mahakama hiyo.
Akizunguzumza na waandishi wa habari baada ya kutoka nje ya jengo la Mahakama Kuu, Lulu alisema anawashukuru watu wote na kuwaomba waendelee kumuombea kwa kuwa hiyo ni dhamana tu,kesi bado inaendelea na safari ni ndefu.
Comments