MELBOURNE, Australia
VICTORIA Azarenka wa Belarus jana alifanikiwa kutetea taji lake la ubingwa wa michuano ya wazi ya tennis ya Australia kwa wanawake baada ya kumbwaga Li Na wa China.
Katika mechi hiyo ya fainali, iliyokuwa na msisimko wa aina yake, Victoria alimshinda Li Na kwa seti 2-1.
Li Na aliianza seti ya kwanza kwa kishindo na kumbwaga Victoria kwa 6-4. Lakini mwanadada huyo wa Belarus alichachamaa katika seti mbili zilizofuata na kushinda kwa 6-4, 6-3.
Kabla ya mchezo huo, Victoria alikuwa hapewi nafasi kubwa ya kutwaa tena taji hilo.
Baadhi ya magazeti ya Australia na hata wasomaji wake, walikuwa wakitoa nafasi kubwa kwa Li Na kuibuka mshindi kutokana na uwezo aliouonyesha katika mechi za hatua ya awali.
Mara baada ya pambano hilo kumalizika, Victoria alijikuta akikaa kwenye kiti uwanjani na kuanza kuangua kilio. Alilazimika kutumia taulo kufuta machozi yake.
Victoria ndiye mchezaji namba moja duniani kwa sasa katika mchezo huo kwa wanawake.
"Nilikuwa na wakati mgumu na sasa najisikia ahueni na mwenye furaha kubwa,"alisema Victoria.
Comments