PORT ELIZABETH, Afrika Kusini
HUWEZI kuamini, lakini ndivyo ilivyokuwa. Cape Verde juzi ilionyesha maajabu baada ya kuichapa Angola mabao 2-1 na kufuzu kucheza robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Katika mechi hiyo ya kundi A iliyochezwa mjini hapa, Angola ilikuwa ikihitaji ushindi ili iweze kufuzu kucheza hatua hiyo na ilikuwa ya kwanza kupata bao.
Mlinzi Neves wa Cape Verde ndiye aliyeizawadia bao Angola dakika ya 33 baada ya kujifunga wakati akiwa kwenye harakati za kuokoa mpira wa hatari uliopigwa kwenye lango la timu yake. Bao hilo lilidumu hadi mapumziko.
Cape Verde ilisawazisha dakika tisa kabla ya mchezo kumalizika kwa bao lililofungwa na beki, Fernando Varela kwa shuti la umbali wa mita zipatazo 17.
Wakati mashabiki wakiamini kuwa pambano hilo lingemalizika kwa sare, Heldon aliifungia Cape Verde bao la pili na la ushindi na kuwafanya wachezaji na viongozi wa timu hiyo wapagawe kwa ushindi.
Angola ililianza pambano hilo kwa kasi, kuliko ilivyokuwa katika mechi zake mbili za awali wakati Cape Verde ilifanya mashambulizi ya kushtukiza.
Cape Verde ilipata nafasi mbili nzuri za kufunga mabao katika kipindi cha kwanza, lakini zilipotezwa na Platini na Ryan Mendes.
Mshambuliaji Manucho alikuwa mwiba mkali kwa mabeki wa Cape Verde, ambao walilazimika kumwekea ulinzi mkali ili asilete madhara kwenye lango lao.
Kocha Luis Antunes wa Cape Verde alisema baada ya mchezo huo kuwa, wanawazawadia ushindi huo wananchi wa visiwa vya Cape Verde.
"Lengo letu katika michuano hii limetimia. Tulitaka kufuzu kucheza robo fainali,"alisema.
Kocha Gustavo Ferrin alisema walilazimika kucheza kwa kushambulia kwa lengo la kuongeza mabao na kusahau kujilinda.Inatoka kwa mdau.
Comments