Na Adnan Hussein, Mogadishu
Wanamgambo wa al-Shabaab wanaondoka mfululizo huko Bardhere katika mkoa
wa Gedo wakati mamia ya askari wa Somalia, wakisaidiwa na majshi ya
Ethiopia, wakisonga mbele kuelekea mjini kudai udhibiti na kurejesha
sheria na utaratibu.
Jeshi la Taifa la Somalia, kama
linavyoonekana hapa likiwa Elasha Biyaha mwezi Novemba 2012,
linatayarisha shambulio kubwa dhidi ya wanamgambo wa al-Shabaab katika
mkoa wa Gedo. [Na Stuart Price/AU-UN IST/AFP]
Mkazi wa eneo hilo Farhan Mohamed Jama alisema aliiona misafara na
magari ya kijeshi ya al-Shabaab yakiondoka kutoka Bardhere kwa muda wa
usiku kadhaa, yakienda magharibi kuelekea Burdubo na Dinsor katika mkoa
wa Bay.
"Kuna mazingira ya kutokuwepo na sheria mjini na al-Shabaab wametangaza
hali ya tahadhari wakijitayarisha na mashambulizi dhidi ya kambi na
ngome zake," Jama aliiambia Sabahi. "Katika baadhi ya mitaa na katikati,
kuna mamia ya wanamgambo wa waasi ambao wameanza kupiga risasi nzito
hewani usiku wa manane wiki hii iliyopita katika jaribio la kuwashitua
wakazi na kuonyesha nguvu zao katika eneo hili."
Siku ya Alhamisi jioni (tarehe 3 Januari), al-Shabaab waliwakamata
viongozi 13 wa dini na kuwashutumu kuwa wanakula njama za kuvikaribisha
vikosi vinavyokaribia, Jama alisema.
Hawa Ahmed Kheyre, muuzaji wa maandazi mwenye umri wa miaka 30 katika
soko la Bardhere, alisema kuwa al-Shabaab wamewaondosha baadhi ya
wapiganaji wao kutoka mjini ili kujitayarisha kwa vita vya msituni na
ulipuaji mabomu.
"Tunaishi katika nyakati za zahama kwa matokeo ya vitisho kutoka kwa
watu wenye siasa kali ambao wamezagaa vijijini kote na milimani ya mkoa
wa Gedo," alisema. "Tunasumbuliwa na mivutano, mauaji na mashitaka
kutoka mikononi mwa wafuasi wa kikundi hiki ambao wamejipenyeza miongoni
mwa watu wa eneo hili."
Diyad Abdi Kalil, afisa wa jeshi la Somalia huko Gedo, alisema kwa kweli
vikosi vya Somalia vinapanga kuishambulia Bardhere na Burdubo, ambazo
bado ziko katika udhibiti wa al-Shabaab, lakini hakusema lini.
Comments