Kocha wa Zambia Herve Renard, amesema ameridhika na jinsi kikosi chake kimejiandaa kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika.
Kocha huyo wa Zambia, amesema kuwa kikosi chake
kiko imara kuliko ilivyokuwa mwaka uliopita, huku wakijiandaa kutetea
kombe hilo nchini Afrika Kusini.
Chipolopolo
inaanza kampeini yake tarehe 21 Januari dhidi ya Ethiopia, baada ya
kushindwa mechi tatu na kutoka sara moja wakati wa mechi zao za
kirafiki.
Licha ya kipigo hicho Renard, ambaye aliongoza
Zambia kushinda kombe hilo kwa mara ya kwanza, mwaka uliopita, amesema
ameridhika na maandalizi yake.
''Naamini kuwa tuko imara kuliko tulivyokuwa mwaka uliopita wakati kama huu'' Alisema kocha huyo.
Renard amesema mwaka uliopita, kabla ya kuanza
kwa fainali hizo alikuwa na wasi wasi kwa kuwa maandalizi yao yaliyokuwa
duni sana.
''Lakini kinyume na matarajio yetu, tulifanya vyema na kushinda kombe hilo'' Aliongeza kocha huyo.
Zambia ilitoka sare ya kutofungana bao lolote na
Morocco, katika mechi ya kirafiki mjini Johannesburg, wiki iliyopita na
kusitisha rekodi ya timu hiyo ya kushindwa.
Kabla ya mechi hiyo Zambia ilishindwa na Angola, Saudi Arabia na Tanzania.
Lakini Renard, licha ya matokeo hayo duni, amesema hana wasi wasi kuhusu kikosi chake.
Zambia inacheza Ethiopia katika mechi yake ya kwanza kisha Nigeria na Burkina Faso katika kundi C.Source BBC.
Comments