YAH: TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA DODOMA KWA VYOMBO VYA
HABARI TAREHE 15/01/2013
Mtu mmoja amefariki Dunia Mkoani Dodoma katika tukio la ajali ya gari kumgonga mtembea kwa miguu na kusababisha kifo.
Marehemu ametambuliwa kuwa ni Mohamed s/o Hassan mwenye umri wa Miaka(110) Mrangi ambaye ni mkazi wa kijiji cha Kalamba kuu Kelema wilayani Chemba.
Uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa Dereva kwa kutokuwa mwangalifu kwa watumiaji wengine wa barabara kwani alikuwa katika mwendo wa kasi katika eneo lenye makazi ya watu kinyume na sheria za usalama barabarani zinavyoelekeza.
Madereva wanatakiwa kujua na kuzingatia ni mwendo gani watumie katika maeneo tofauti wanayopita, kama Kifungu namba 51, kifungu kidogo cha 8 (a) cha sheria ya Usalama barabarani ya Mwaka 1973 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 sura ya 168 ambayo inatamka bayana kwamba mtu yeyote anayetumia chombo cha moto barabarani haruhusiwi kuendesha chombo hicho zaidi ya spidi 50 kwenye makazi ya watu.
Napenda kutoa wito kwa madereva wote kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za usalama Barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima, ambazo hulipunguzia taifa nguvu kazi.
Mtuhumiwa anashikiliwa na Jeshi la Polisi na atafikishwa mahakamani pindi uchunguzi utakapokamilika.
DAVID MISIME - ACP
KAMANDA WA POLISI MKOA WA DODOMA
Comments