Rais wa Marekani Barack Obama akiwa na Makamu wa Rais Joe Biden punde
baada ya Baraza la Seneti kupitisha sheria zilizonusuru bajeti ya nchi
hiyo
Wabunge nchini Marekani wamekuwa kwenye mvutano mkali punde tu baada ya
kumalizika kwa sherehe za Noeli na kuwalazimu kurejea haraka kuendelea
na mchakato wa kupitishwa kwa sheria hizo ili kunusuru bajeti ya
serikali.
Wasiwasi mkubwa ulikuwa umetanda kutokana na pande mbili zenye wabunge
wengi Republican na Democrats kutunishiana misuli kutokana na kila
upande kushikilia msimamo wake hatua ambayo imeliingiza taifa hilo
kwenye hofu ya kutetereka kiuchumi.
Makamu wa Rais Joe Biden ndiye ambaye ameshiriki kwa kiasi kikubwa
kuhakikisha ananusuru upitishwaji wa sheria hizo baada ya kukutana na
Wabunge wa Republican ambao walikubali kuweka tofauti zao na Democrats
kando na kuangalia maslahi ya Umma.
Congress imepitisha sheria hizo baada ya hapo awali Bunge la Seneti
kuridhia hatua kama hiyo kwa kupiga kura za ndiyo 257 dhidi ya kura za
hapana 167 na hivyo kuonesha mwelekeo mwema.
Licha ya kupitishwa kwa sheria hizo lakini kumekuwa na mfarakano wa
kisiasa huku wabunge wa Chama Cha Republican wakitaka marekebisho kadhaa
yafanyike ili sheria hizo ziwe na manufaa kwa wananchi.
Rais wa Marekani Barack Obama amekiri kufurahishwa na hatua ambayo
imefanywa na wabunge wa nchi hizi na kuahidi atasaini sheria hiyo ambayo
itaongeza kiwango cha ulipaji kodi kwa asilimia mbili kwa matajiri.
Comments