Skip to main content

Wachuuzi wachukiana na mamlaka, biashara katikati ya Nairobi


Na Bosire Boniface, Nairobi
Antony Macharia anaichukulia njia ya waenda kwa miguu katika mtaa wa Ronaldo Ngara wa Nairobi kama ofisi yake.
Wachuuzi wakiuza vyombo kandokando ya barabara ya Moi katika mtaa wa biashara katikati ya Nairobi. Wachuuzi aghalabu hutumia mitaa hiyo wakati wa jioni, wakisababisha msongamano wa magari barabarani. [Bosire Boniface/Sabahi]
Kinjia kilichonyooka kwa umbali wa kilometa moja kandokando ya mtaa katika Wilaya ya Biashara ya Katikati ya Nairobi (NCBD) imejazwa na wachuuzi wanaouza bidhaa mbalimbali kutoka saa 10.00 jioni wakati ofisi zinapofungwa hadi kuzidi saa 4.00 usiku.
Macharia amekuwa akiuza viatu mahali hapo kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitatu kusaidia familia yake ya watu wanne. Biashara hii imenipa fursa ya kununua sehemu ya ardhi na gari, pamoja na kusomesha watoto wangu na kusaidia wanafamilia wengine," aliiambia Sabahi.
Hata hivyo, Macharia na wachuuzi wengine hawaruhusiwi kisheria kuuza bidhaa zao hapo.
Mary Wekesa, mwenye umri wa miaka 34 na mama wa watoto watatu ambaye anauza njegere, alisema polisi wa jiji hutumia mbinu zisizopendeza kutekeleza kanuni ambazo zinazuia wamachinga mitaani kutokufanya biashara katika NCBD.
"Maofisa wa polisi na viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Nairobi walitupiga, walikamata biashara zetu, na kutukamata kila walipotukuta katika maeneo yaliyozuiliwa," aliiambia Sabahi.
Alisema Soko la Wachuuzi la Muthurwa, ambako wachuuzi wanaruhusiwa kufanya biashara zao, ni mbali na katikati ya mji, na wafanyakazi wengi wa mjini hawako tayari kufunga safari kwenda huko.

Comments