Balozi wa Tanzania katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe, Sylvester Mabumba (wa pili kutoka kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji wa Comoro, Bw. Said Mohamed Omar (wa pili kutoka kushoto), Mkurugenzi wa vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media Group pamoja na wajumbe waliofuatana nao katika ziara maalum ya kufungua na kuzitangaza fursa zilizopo Tanzania na Comoro.
WATANZANIA WAHIMIZWA KUCHANGAMKIA FURSA COMORO
Balozi wa Tanzania
katika Muungano wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Sylvester M. Mabumba alipokea
ujumbe wa Clouds Media Group uliowasili visiwani humo tarehe tarehe 20
Januari 2017 kwa ziara maalumu ya siku tatu ikiwa na lengo la
kushirikiana na Ubalozi kuzitangaza fursa mbalimbali zinazopatikana
Visiwani humo kwa Watanzania.
Ujumbe huo wa Clouds
Media Group ukiongozwa na Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji, Bw. Ruge
Mutahaba uliwasili Comoro kufuatia mualiko wa Ubalozi wa Tanzania hapa
Comoro ambapo lengo lake lilikuwa ni kuja kufanya tathamini ya kuzindua
Jukwa la Fursa (FURSA EXPO) Visiwani Comoro kama sehemu ya kuendeleza
kampeni za kuwapatia vijana wa Kitanzania taarifa muhimu kuhusiana na
fursa za uwekezaji na biashara.
Ubalozi wa Tanzania
Visiwani Comoro kwa kushirikiana na Ujumbe wa Clouds Media Group
umelenga ifikapo mwezi Aprili 2018 kupanua mianya ya uwekezaji nchini
Comoro pamoja na kuhakikisha kwamba masoko ya uhakika yanapatikana kwa
ajili ya bidhaa za Tanzania hasa katika kipindi hiki ambapo Uchumi wa
Tanzania unaelekea kuwa ni uchumi wa Viwanda.
Aidha, Mhe. Balozi
akiwa ameambatana na ujumbe wa Clouds Media Group alipata fursa ya
kuonana na kufanya mazungumzo na wadau kutoka sekta mbalimbali za
Serikali ya Comoro, Mashirika ya Umma na Sekta Binafsi. “Serikali ya
Tanzania itaendelea kufungua maeneo mapya ya ushirikiano sambamba na
kuhakikisha vijana wananufaika na ushirikiano baina ya nchi na nchi
ulioanzishwa na mataifa yao” alisema Mhe. Balozi
Aidha, Mhe. Balozi
alielezea anataraji ziara hiyo italeta matokeo chanya na kwamba
kuzinduliwa kwa jukwaa la FURSA EXPO ni sehemu mojawapo ya utekelezaji
wa Sera ya Mambo ya Nje ambayo inalenga kwenye Diplomasia ya Uchumi na
kwamba kupitia jukwaa hilo bidhaa za Tanzania zinauhakika wa kuingia
kwenye Soko la Comoro kwani nchi ya Comoro inaitegemea Tanzania kwa
kiasi kikubwa katika mahitaji yake mbalimbali.
Pia ujumbe wa Clouds
Media Group ulitumia nafasi hiyo kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu
wa Mamlaka ya Uwekezaji Visiwani Comoro, Ndg. Said Mohamed Omar,
Mkurugenzi Mkuu Ofisi ya Kitaifa ya Utalii, Ndg. Mouzamildine Youssouf
pamoja na Mkurugenzi wa Uhamasishaji wa Vijana. Katika mazungumzo hayo,
wajumbe walionesha nia ya kutaka kushirikiana kwa pamoja katika
kuendesha kampeni itakayoibua maeneo muhimu ya kimkakati ambayo Vijana
wa Kitanzania na wale wa KiComoro wanaweza kushirikiana.
Naye Bw. Ruge Mutahaba kwa upande wake
alieleza kufurahishwa na fursa mbalimbali zinazopatikana Comoro na
kuahidi kuendelea kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania Visiwani hapa
kuhakikisha kwamba FURSA EXPO Comoro inafanikiwa na kuleta matokeo
chanya kwa lengo la kuinua uchumi wa vijana wa Kitanzania na wa
KiComoro.
Balozi wa Tanzania katika Muungano wa
Visiwa vya comoro pamoja na Wajumbe kutoka clouds Media Group wakiwa
katika mazungumzo ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii
Comoro, Bw. Mouzamildine Youssouf.
Comments