Imeelezwa maafisa wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo,wanakabiliana na wapinzani wa rais Joseph Kabila
Waandamanaji jijini Kinshasa Desemba 31 2017
Umoja wa Mataifa umesema umesikitishwa na namna maafisa wa usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanavyokabiliana na wapinzani wa rais Joseph Kabila.
Kauli hii inakuja baada ya makabiliano kati ya maafisa wa usalama na waandamanaji mwisho wa mwaka uliopita katika miji mbalimbali kushinikiza kujiuzulu kwa rais Joseph Kabila.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu (OHCHR) yenye makao yake jijini Geneva, imesema maafisa wake wamezuiwa kwenda kwenye vyumba vya kuhifadhi maiti, hospitali na vituo vya polisi, kujionea matokeo ya makabiliano hayo.
Maandamano hayo yalipangwa na viongozi wa Kanisa Katoliki, ambao pia wamelaani hatua ya polisi kuamua kuvunja maandamano hayo.
Waandamanaji saba waliuawa na wengine kujeruhiwa na sasa umoja wa Mataifa unasema, kuwa huenda idadi ya watu waliopoteza ikawa kubwa zaidi.
Serikali ya DRC imekuwa ikisema kuwa hakuna aliyepoteza maisha katika maandamano hayo.
Kumekuwa na shinikizo kwa rais Kabila kuachia madaraka, na kutangaza kutowania urais wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika mwisho wa mwaka huu.
Comments