Mapinduzi ya Zanzibar yalitokea mwaka 1964 ili kumuondoa madarakani Sultani wa Zanzibar na serikali yake, iliyoundwa hasa na Waarabu, na hatimaye kuweka uongozi mikononi mwa Waafrika, ambao ndio wengi visiwani humo (230,000 hivi), kwenye bahari ya Hindi, karibu na pwani ya Tanganyika.
Usultani wa Zanzibar ulikuwa umepewa na Uingereza uhuru wake mwaka 1963. Kabla ya hapo, Waarabu walikuwa wamefaulu kudumisha katika mfululizo wa chaguzi utawala waliokuwa nao tangu zamani za Zanzibar kuwa chini ya Usultani wa Omani.
Chama cha Afro-Shirazi Party (ASP), kilichowakilisha hasa Waafrika, kilipoona kwamba bungeni kina viti vichache ingawa kilipata 54% za kura katika uchaguzi wa Julai 1963, kilipatana na chama cha mrengo wa kushoto Umma Party.
Tarehe 12 Januari 1964 asubuhi na mapema, mwanachama wa ASP John Okello (1937-1971 ?) kutoka Uganda aliongoza wanamapinduzi 600–800 wa kisiwa kikuu cha Unguja kushinda polisi wa nchi na kuteka silaha zao. Halafu walielekea Zanzibar Town walipompindua Sultani Jamshid bin Abdullah na serikali yake. Waliokufa katika mapigano wamekadiriwa kuwa 80 hivi tu.
Kumbe yalifuata kwa siku kadhaa (labda hadi tarehe 20 Januari) maangamizi ya kimbari dhidi ya Waarabu (waliokuwa 50,000 hivi) na Waasia wa Asia Kusini (waliokuwa 20,000 hivi); hakuna hakika kuhusu idadi ya waliouawa: makadirio yanataja kuanzia mamia kadhaa hadi 20,000.
Kiongozi wa ASP Abeid Karume, asiyekuwa na msimamo mkali akawa rais wa kwanza wa nchi, na wanachama wa Umma party walipewa nafasi serikalini. Kufikia Machi Okello alikuwa ameshawekwa pembeni na kufikia Aprili kikosi chake kimeshanyang'anywa silaha.
Mwelekeo wa Kikomunisti wa baadhi katika serikali mpya uliogopesha nchi za Magharibi. Kwa kuwa Zanzibar ilikuwa chini ya athari ya Uingereza, serikali yake iliandaa mipango kadhaa. Hata hivyo, hofu ya kuundwa serikali ya Kikomunisti haikutimia kamwe, na kwa kuwa wananchi wa Uingereza na Marekani waliweza kuhama bila shida, mipango hiyo haikutekelezwa.
Wakati huo nchi za Kikomunisti za China, Ujerumani Mashariki na Umoja wa Kisovyeti zilianzisha mahusiano ya kirafiki na serikali mpya ya Zanzibar kwa kuitambua rasmi na kwa kutuma washauri.
Karume alifanikisha majadiliano ya kuunganisha Zanzibar na Tanganyika ili kuunda hatimaye muungano wa Tanzania; vyombo vya habarivilitafsiri muungano huo kuwa juhudi za kuzuia Ukomunisti kugeuza Zanzibar.
Mapinduzi yalikomesha miaka 200 ya utawala wa Waarabu Zanzibar, na yanaadhimishwa kila mwaka kama sikukuu ya taifa zima la Tanzania.
Comments