Liverpool jana imeweka historia mpya baada ya kukutana katika pambano na klabu ya Manchester City kwa kuiadhibu 4-3 kwenye mchezo mkali wa Premier League uliochezwa Anfield.
Kabla ya mchezo wa leo, Manchester City ilikuwa imecheza mechi 22 za Premier League na kushinda michezo 20 huku ikitoa sare mara mbili.
Liverpool ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Alex Oxlade-Chamberlain dakika ya 9 lakini Leroy Sane akaichomolea City dakika ya 44 na kufanya timu hizo ziende mapumziko zikiwa nguvu sawa.
Kipindi cha pili Liverpool ikapata mabao matatu mfululizo kupitia kwa Roberto Firmino dakika ya 59, Sadio Mane dakika ya 61 na Mohamed Salah dakika ya 68.
Wakati wengi wakiamini Liverpool imeshinda mchezo huo kirahisi, City wakacharuka na kupunguza mabao mawili ukingoni mwa mchezo wafungaji wakiwa ni Bernardo Silva dakika ya 82 na Ilkay Guendogan dakika ya 90.
Dakika ya mwisho katika nne zilizoongezwa kufidia muda wa majeruhi, Manchester City wakapoteza nafasi nzuri ya kusawazisha baada ya Aguero kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Kevin De Bruyne huku kipa na mabeki wa Liverpool wakiwa hawana la kufanya, lakini mpira ukatoka nje kwa sentimita chache.
Comments