KIKOSI cha Yanga, leo kitapambana na URA ya Uganda katika mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Mapinduzi inayoendelea kutimua vumbi mjini Unguja huku kocha wa Simba akiwapa mbinu. Mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa itafanyika kwenye Uwanja wa Amaan mjini Unguja.
Hata hivyo, Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ambaye hivi karibuni alifungashiwa virago na klabu hiyo, ameitaka Yanga kuhakikisha inacheza kwa nidhamu kubwa na URA kama inataka kuibuka na ushindi.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka kwao Cameroon, Omog alisema, kuwa wachezaji wa URA wanacheza kwa nidhamu kubwa na kwa ushirikiano wa hali ya juu ndiyo maana katika michuano hiyo timu hiyo inaonekana kuwa ni ngumu.
Alisema wachezaji wa Simba walipoteza umakini katika mechi zao na kushindwa kuzitumia vizuri nafasi walizokuwa wakizipata jambo ambalo ndilo limesababisha washindwe kuibuka na ushindi katika michezo yake. Amesema kwenye mechi dhidi ya URA walipoteza umakini ndiyo maana walifungwa kirahisi.
“Nimesikitishwa na kitendo cha Simba kuondolewa katika michuano hiyo lakini kila mtu anapaswa kukubaliana na matokeo hayo na hivyo ndivyo mchezo wa soka ulivyo. “Wachezaji wa Simba walipoteza kidogo umakini katika mechi hiyo ambayo video yake nimeiona leo (jana) kupitia mtandao baada ya kutumiwa na rafiki yangu mmoja ndiyo maana walifungwa japokuwa walicheza vizuri.
“Kwa hiyo, Yanga wanatakiwa nao kuwa makini katika mechi hiyo, kila mchezaji aingie uwanjani kupambana na kuyafanya majukumu yake kwa ufanisi mkubwa kama kweli wanataka kuibuka na ushindi, nimewaona URA ni wazuri na wanacheza kwa akili sana. “Yanga watafanya kosa kama watawaachia nafasi ya kutawala mchezo huo,” alisema Omog ambaye mwaka jana aliongoza timu hiyo kutinga fainali ya michuano hiyo lakini ikifungwa na Azam FC
Comments