WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza Ofisa Ushirika wa Manispaa ya Musoma, Yunia Wiga kufuatilia upotevu wa sh. milioni 320 za Imara SACCOS na atakayebainika kuhusika ashughulikiwe.
Waziri Mkuu Kassim Maja
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Ofisi ya Waziri Mkuu, alitoa kauli hiyo jana jioni alipopokea malalamiko ya wanachama wa SACCOS hiyo kupitia mabango waliyoyawasilisha katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mukendo mjini Musoma.
Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Mara kwa ziara ya kikazi ya siku sita, alimuagiza ofisa huyo kukutana na uongozi na wanachama wa SACCOS hiyo leo mchana na kisha kumpa majibu juu ya upotevu wa fedha hizo pamoja na sh. milioni 40 za hisa ifikapo Januari 20, 2018.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Musoma Bibi Fidelica Myovella kuhakikisha anatenga fedha kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi mbalimbali waliopisha miradi ya maendeo katika Manispaa hiyo.
Waziri Mkuu alisema siyo vizuri kwa halmashauri kuchukua maeneo ya wananchi kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maendeleo kama barabara, standi na kisha kukaa muda mrefu bila ya kuwalipa fidia zao.
Aliyasema hayo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi waliopisha ujenzi wa kituo cha daladala cha Bweri ambao hawajalipwa fidia zao tangu mwaka 2013. Mkurugenzi huyo aliahidi kuanza kulipa madeni hayo kuanzia mwezi Januari, 2018.
Awali, Mbunge wa jimbo la Musoma Mjini, Vedastus Mathayo aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli kwa kutekeleza baadhi ya ahadi alizozitoa wakati wa kampeni ikiwemo ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Mathayo alisema wananchi wa jimbo hilo kwa muda mrefu walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa utekelezaji wa ahadi hiyo.
Mbali na mradi wa maji pia Serikali inatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo ikiwemo ya ujenzi wa barabara za mitaa kwa kiwango cha lami pamoja na ukarabati wa kiwanja cha ndege unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Waziri Mkuu alisema ahadi zote zilizopo kwenye ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015 na zile zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli zitatekelezwa, hivyo wananchi waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Comments