MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Taifa (CCM) bara, Philip Mangula amesema anawapenda wanaoikosoa CCM kwakuwa wamekuwa wakichangia kurekebisha mapungufu yao na kujiimarisha.
Philip Mangula kushoto akisalimiana na makada wa chama cha CCM
Mangula ameyasema hayo leo Chanika jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi iliyofanyika ya kumpokea mwanachama mpya aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya wadhamini wa Chadema, Muslimu Hassanali.
Mangula amesema siasa za ukosoaji ni kutoa mawazo na wengine wakayarekebisha lakini upinzani wamekuwa wakosoaji kwa kubeza.
“Kukosoa ni silaha ya mapinduzi, kukiri kosa na kusahihisha ni jambo la msingi wenzetu wamekuwa ni vyama vya kukosoa CCM ninawapenda sana na kuwaunga mkono kwani wao wanakosoa kwa kubeza lakini inatusaidia kujirekebisha,”amesema Mangula.
Amesema CCM hukosoa kupitia vikao maalum ndani ya Chama kwa kuangalia katiba yao na kuirekebisha kwa mawazo mapya.
“ Mlilalamikia kwa nguvu kuhusu mafisadi, mikataba mibovu, rasilimali za nchi lakini chini ya JPM hayo yote yametekelezwa hamna cha kukosoa sasa,”amesema Mangula.
Amesema CCM inaongozwa kwa mujibu wa Katiba na wana ahadi zao 189 ambazo wanazitekeleza kwa vipaumbele na umuhimu wake hivyo wapinzani wasiwapangie agenda ya kufanya.
Akimzungumzia Hassanali, Mangula amesema“ Ipo minong’ono pembeni inayosema sisi tumekuwa tukiwanunua wapinzani…fedha hizo hatuna kwani waumini wanapohama makanisa wanapewa fedha na nani zaidi ya kukubali kinachofanyika upande mwingine ?,”amehoji Mangula.
Kwa upande wake, Hassanali amesema, aliitumikia Chadema kwa miaka 15 na amejifunza mambo mengi akiwa ndani ya chama hicho.
“ Sijashawishiwa na mtu...zaidi ya mwaka mmoja nimetafakari maisha yangu ndani ya Chadema lakini nikaona niweke nafsi yangu nyuma nitangulize maslahi ya jamii mbele.
“Nimeamua kuacha kuwa mkosoaji wa CCM na badala yake niungane na rais kuleta maendeleo ya nchi…nitashiriki kuleta maendeleo na si kuichafua serikalim,”amesema Hassanali.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM, Humphrey Polepole amesema wanachama wanaohamia CCM hupata vitisho na hata kufanyiwa fujo nakumuomba Mangula awasaidie.
"Wanachama hao wamekuwa wakipokea vitisho, kuvunjwa mioyo na kutishiwa hivyo uhakikishe wanalindwa wasipate vitisho na kuonewa kwani tabia yao, "amesema.
- Get link
- X
- Other Apps
- Get link
- X
- Other Apps
Comments