Mahakama ya Rufaa
imesema hakuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la Longido iliyopo mahakamani hapo.
Mahakama imetoa kauli
hiyo wakati Chadema ikiilalamikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhusu
kufanyika uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo kwa madai kwamba kuna kesi
mahakamani hapo.
Uchaguzi huo mdogo
ulifanyika baada ya aliyekuwa mbunge wa Longido kwa tiketi ya Chadema, Onesmo
ole Nangole ushindi wake kutenguliwa na Mahakama Kuu.
Mara kadhaa Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe na Ole Nangole wamekaririwa na vyombo vya habari
wakidai kwamba kuna rufaa katika Mahakama ya Rufani.
Viongozi hao wamekuwa wakiilalamikia NEC kuwa
iliendesha uchaguzi mdogo katika jimbo hilo wakati rufaa ya kupinga hukumu ya
Mahakama Kuu iliyomvua ubunge Ole Nangole ikiwa haijatolewa uamuzi.
Mahakama ya Rufaa
imesema uchaguzi mdogo uliofanyika Longido ulikuwa halali kwa kuwa hakuna rufaa
yoyote iliyoko mahakamani hapo.
Naibu Msajili wa
Mahakama ya Rufaa, Elizabeth Mkwizu amesema hakuna rufaa yoyote kupinga hukumu
ya uchaguzi wa Longido iliyoko mahakamani hapo, bali kuna maombi.
“Hapa hatuna rufaa ya uchaguzi wa Jimbo la
Longido, bali kuna maombi ya kuongezwa muda wa kuwasilisha ‘notice of appeal’
(taarifa ya kusudio la kukata rufaa).
“Maombi si rufaa, kwa hiyo haya maombi
yasingeweza kusimamisha shughuli za uchaguzi.
” Kwa mujibu wa ratiba
ya vikao vya Mahakama ya Rufaa, maombi hayo yamepangwa kusikilizwa na Jaji
Jacob Mwambegele Februari 5.
Wakati wa usikilizwaji
wa maombi hayo, mwombaji kupitia kwa mawakili wake atalazimika kutoa sababu za
kuiridhisha Mahakama ni kwa nini alichelewa kuwasilisha taarifa ya kusudio la
kukata rufaa.
Ikiwa Mahakama
haitaridhika na sababu zake, itatupilia mbali maombi hayo lakini ikiridhika
nazo itamruhusu kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Baada ya kuwasilisha
taarifa hiyo, atasubiri kupata kumbukumbu za rufaa, yaani nyaraka
zitakazohusika kwenye rufaa yake, ikiwamo hukumu anayoilalamikia, mwenendo wa
kesi ya msingi na vielelezo vilivyotumika.
Akipata nyaraka hizo, ndipo atakapowasilisha
rufaa kamili, yaani sababu za kwa nini anapinga hukumu iliyomvua ubunge wa
jimbo hilo, na upande wa pili (wajibu rufaa) nao utawasilisha hoja zake na
baada ya Mahakama kusikiliza hoja za pande zote ndipo itatoa hukumu.
Ole Nangole alivuliwa
ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha Juni 29, 2016 kutokana na kesi ya
uchaguzi iliyofunguliwa na aliyekuwa mgombea wa kiti hicho kwa tiketi ya CCM,
Dk Steven Kiruswa akipinga ushindi wake.
Baada ya Mahakama
kumvua ubunge, Ole Nangole kupitia mawakili John Materu na Dancan Oola
aliwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo.
Hata hivyo, taarifa
hiyo ya kusudio la kukata rufaa ilitupiliwa mbali na Mahakama kutokana na
kasoro za kisheria. Baada ya kutupiliwa mbali, kwa kuwa muda wa kisheria wa
siku 14 za kuwasilisha kusudio la kukata rufaa ulikuwa umeshaisha, waliwasilisha
maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha taarifa hiyo.
Comments