* Atosha Kissava naye kushiriki
Na Mwandishi Wetu
TAMASHA
la Pasaka linalofanyika kila mwaka kwa kuandaliwa na Kampuni ya Msama
Promotions ya Dar es Salaam, linazidi kupanuliwa wigo mwaka huu kwa
kushirikisha wasanii nguli.
Akizungumza
na Jambo Leo, Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya
tamasha hilo, Alex Msama alisema mwimbaji Atosha Kissava kutoka Mkoa wa
Iringa amekuwa wa tatu kuthibitisha kushiriki tamasha hilo.
"Kissava
ambaye ana kundi lake la muziki wa injili, anakuwa mshiriki wa tatu
kuthibitisha kushiriki tamasha la Pasaka baada ya Upendo Kilahiro na
Upendo Nkone," alisema Msama.
Tamasha
hilo linatarajiwa kurindima Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Aprili 8
mwaka huu na pia litafanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma
Aprili 9 mwaka huu.
Kissava
hivi sasa anatamba na albamu ya Nainua Macho Yangu Juu yenye nyimbo za
Alpha na Omega, Unaweza, Nifanane na Wewe, Nibariki na Mimi, Kwake
Yesu, Njooni Njooni, Yatima na Nainua Macho uliobeba jina la albamu.
"Tunaboresha
mambo mengi kuliko miaka iliyopita, waimbaji mwaka huu watakuwa
wachache kiasi wakiwamo wa kutoka mataifa mengine ya Afrika... hiyo
yote tumefanya ili kukidhi matakwa ya wapenzi wa muziki wa injili.
"Mbali
na Tanzania, pia tutakuwa na waimbiaji kutoka Kenya, Uganda, Zambia,
Afrika Kusini, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo katika tamasha
hilo la nyimbo za injili za kumsifu Mungu.
"Mwaka
jana hatukuandaa tamasha la Krismasi, hivyo nguvu zote tumezielekeza
katika tamasha hili la Pasaka... Wapendwa wajiandae kushiriki kwa wingi
kwani watashiba kiroho kwa vile kutakuwa na waimbaji wengi wenye hamasa
ya kiroho," alisema Msama.
Msama
aliyechangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa muziki wa injili akiwa mwasisi
wa matamasha ya injili nchini, alisema lengo la kuwajumuisha wasanii
hao ni kutaka kulifanya tamasha hilo kuwa tofauti na miaka mingine.
Alisema
tamasha hilo litakuwa na kiingilio cha chini zaidi (kitatangazwa
baadaye), ili kila mmoja ahudhurie na kupata baraka kutoka kwa waimbaji
hao wanaomsifu Mungu.
"Waimbaji
wengi maarufu wa muziki wa injili watakuwepo, tumejipanga vizuri
kuhakiksha tamasha hili linakuwa gumzo kila mahali," alisema.
Comments