Ndugu zangu,
GAZETI
la Mwananchi Jumapili lilibeba kwenye kurasa ya mbele habari yenye
kichwa; “ Wabunge CCM wagoma kukutana na Kikwete.” Kwamba wajipanga
kukwamisha muswaada wa mabadiliko ya Katiba.
Yumkini
habari ile ilikuwa ni ‘burudani’ tu ya wasomaji kwa siku ya Jumapili.
Maana, tunaojaribu kufuatilia siasa za nchi hii tunafahamu, kuwa jambo
hilo haliwezekani. Nitafafanua.
Na ‘ The Citizen’ leo Jumanne kwenye kurasa ya mbele limebeba habari hii; “Katiba; Chadema, CCM in tug-of-war”.
Mwandishi
Lucas Liganga anatutoa kwenye reli kwa kuripoti kuwa wachambuzi wa
masuala ya kisiasa wanadai kuwa mvutano kati ya Chadema na CCM unaweza
kututoa kwenye reli mchakato wa kupata Katiba Mpya.
Swali ni hili; Ni nani aliyetoka kwenye reli?
Nahofia, kuwa wanaotajwa kuwa wachambuzi wa mambo ya kisiasa ndio waliotoka kwenye reli.
Nionavyo;
mchakato wa mabadiliko ya Katiba bado uko kwenye reli kwa vile
aliyeuweka kwenye reli bado anataka uwepo kwenye reli, ni JK.
Ndugu zangu,
Kwenye
nchi za Kifalme, baada ya Mungu Mfalme ndiye anayefuatia. Insha-allah
ina maana ya ’ neno la Mungu’ ama utashi wa Mungu. Na kwenye nchi ya
Kifalme, basi, baada ya ’ Utashi wa Mungu’ unafuata ’ Utashi wa Mfalme’.
Na
katika ’ Jamhuri’ kwa maana nchi zinazoongozwa na ’ Rais’ utaratibu ni
huo huo; kwamba baada ya ’ utashi wa Mungu’ kinachofuata ni ’ utashi wa
Rais’.
Ndio,
katika mifumo hii ya utawala; mfalme na Rais wana nguvu nyingi
zinazoweza kukaribiana na za Mungu. Ndio maana tunataka mabadiliko ya
Katiba ambayo, mbali ya mambo mengine, yatapunguza nguvu za Rais.
Katika dunia ya sasa, Rais hapaswi kuwa juu ya kila kitu.
Kinachoshangaza kwa wabunge wa CCM
Kama
kuna wanaodhani hoja ya mabadiliko ya Katiba ni ya Chadema wanakosea.
Mchakato wa kutaka mabadiliko ya Katiba n i hoja ya wananchi hata kabla
ya kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Akina James Mapalala
bado wako hai, wafuatwe waeleze historia ya harakati za kuleta
mabadiliko ya Katiba katika nchi hii.
Wabunge wa CCM wafanye nini?
Tofauti
na mazoea ya huko nyuma. Katika hili la Katiba na namna iliyo bora ya
kuendesha mchakato huu ni suala ambalo haliepukiki kuwahusisha wananchi
na watu wa vyama vya upinzani.
Mwenyekiti
wao Kikwete ameshaliona hili. Kwa kulisimamia hili la Katiba kwa jinsi
alivyoyapokea mapendekezo ya wadau wengine nje ya CCM , Kikwete
anajitengezea mazingira ya kukubalika zaidi na Watanzania, na pia
kuheshimiwa zaidi kama kiongozi wa nchi. Maana, atakuwa amekisikia
kilio cha wengi.
Kwa
wabunge wa CCM kumwekea ‘ mawe barabarani’ Mwenyekiti wao kimsingi
wataharakisha kazi ya kuchimbwa kwa makaburi yao ya kisiasa na ya chama
chao pia ifikapo mwaka 2015.
Katika
mazingira ya sasa. Wabunge CCM, kwa kuamini kuwa Mwenyekiti wao wa
chama ‘ kamwaga mboga’, nao wanaweza kuamua ‘kumwaga ugali’ kwa kupitia
Bunge. Lakini, Mwenyekiti wao ana uwezo wa kwa haraka, kupika vyote
viwili; mboga na ugali, akala na akashiba. Wabunge wake hawatakuwa na
uwezo huo. Lakini, JK , katika saa 24 zijazo, kwa kadri upepo wa
kisiasa utakavyovuma, anaweza pia kufanya kisichotarajiwa; anaweza, ama
kulivunja Bunge au kulivunja Baraza la Mawaziri.
Ndio
maana, jana tumemsikia Jenister Mhagama wa CCM akiwaambia wabunge wa
CCM simu zao ziwe wazi na wasiwe mbali pindi watakapohitajika.
Mwenyekiti wao ametua Dodoma jana.
Kwa
wabunge wa CCM, hawawezi kwenda kinyume na ‘ utashi’ wa Mwenyekiti tena
unaotokana na hekima yake ya kuwasikiliza anaowaongoza.
Kinatachoanyika
sasa ni ‘ face-saving’- kwa wabunge wa CCM kutengeneza sentesi za ‘
kuziba nyuso’ na huku wakimpongeza Mwenyekiti wao kwa busara na hekima
zake. Na anastahiki.
Na Mhagama huyo huyo jana ameongea na gazeti la Chama chake, Uhuru. Ni kwenye gazeti la Uhuru leo tunapoupata ukweli.
Na
ukweli ni huu; “ Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama , amekanusha
habari zilizoandikwa na baadhi ya vyombo vya habari nchini mwishoni mwa
wiki iliyopita kuwa, wabunge hao walipanga mkakati wa kukwamisha
muswaada wa Katiba uliotarajiwa kuwasilishwa bungeni jana na kukutana
na Rais Kikwete. ( Uhuru, Februari 7, 2012)
Na tusubiri tuone, kama Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama, naye amelidanganya gazeti la Chama chake.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam.
Comments